Ufaransa yaongeza majeshi yake CAR | Matukio ya Afrika | DW | 07.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ufaransa yaongeza majeshi yake CAR

Operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Ufaransa imezinduliwa katika Jamhuri ya Afrika ya kati, huku rais wa Ufaransa akitangaza idadi ya wanajeshi itaongezwa baada ya mauaji ya raia katika ghasia Alhamisi wiki hii.

Jeshi la Ufaransa

Jeshi la Ufaransa

Inaripotiwa kuwa wanajeshi walio watiifu kwa rais aliyeondolewa Francois Bozize, walihusika katika mashambulizi kadhaa yaliyotokea kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika ya kati.

Jana Ijumaa Ufaransa ilipeleka takriban wanajeshi wake 1000 katika Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati ambayo shirika la msalaba mwekundu limesema mapigano ya kidini yamesabaisha mauaji ya watu 300.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande

Rais wa Ufaransa Francois Hollande

Hata hivyo idadi hiyo inatofautiana na ile ya madaktari wasio na mipaka MSF walioweka idadi ya waliofariki kuwa 92.

waliojeruhiwa na kusajiliwa katika hospitali moja mjini Bangui walifikia 55 huku miili mingine 80 ikihesabiwa ndani ya misikiti na maeneo ya karibu.

Wanajeshi hao wa Ufaransa walionekana wakishika doria katika barabara za mji wa Bangui, hii ikiwa ni juhudi ya kutuliza wasiwasi katika taifa hilo koloni lake la zamani ambalo limepokea wanajeshi 1200 wa kulinda amani walioridhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama lapitisha uamuzi

Wiki hii pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kuridhia vikosi vya Ufaransa kujiunga na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika katika nchi hiyo. Serikali ya Afrika ya Kati imekaribisha hatua hiyo inayonuia kurejesha utulivu katika mji mkuu Bangui.

Hapo jana Ujerumani ilisema iko tayari kutoa msaada wake wa kiufundi kwa vikosi vya Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wanachama wa UN

Wanachama wa UN

Katika juhudi za kutafuta mahali pa kujikinga kutokana na mapigano yanaotokea mara kwa mara katika Jamhuri hiyo, maelfu ya wakaazi wamekusanyika karibu kabisa na uwanja wa ndege wa Bangui ambapo vipo vikosi vya Ufaransa na vile vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika.

Jamhuri ya Afrika ya kati iliingia katika mzozo tangu waasi walioungana pamoja na kuunda kundi la seleka walipopindua serikali mwezi Machi na kumuweka kiongozi wao Michel Djotodia, kuiongoza nchi hiyo kama rais wa kwanza wa kiislamu katika taifa hilo lililo na idadi kubwa ya wakristo.

Viongozi wa Afrika wajadili Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wakati huo huo mjini Paris, rais wa Ufaransa Francois Hollande, Mkuu wa Umoja wa Mataifa na viongozi 40 kutoka mataifa ya Afrika walifungua mkutano ambapo suala la Afrika ya kati ndio mada inayozungumziwa zaidi.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon

Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon

Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesema mataifa ya Afrika hayapaswi kukubali nchi ya Afrika ya kati kukumbwa na machafuko zaidi na kutawaliwa na magaidi.

Kwa upande wake Hollande amesema Afrika inapaswa kujihakikishia usalama wake ili kuchukua udhibiti wa mustakbali wake huku akiahidi kuwa Ufaransa itasaidia kwa kuunda kikosi maalum cha kiafrika kupambana na hali halisi na kusema pia itatoa mafunzo kwa wanajeshi takriban elfu 20,000 kila mwaka.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba