1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yakataa kumsaidia Rais Bozize

Admin.WagnerD3 Januari 2013

Ufaransa imekataa ombi la rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kusaidia kuwarudisha nyuma waasi wanaotishia kuiangusha serikali yake, huku Marekani ikiamua kufunga ubalozi wake nchini humo.

https://p.dw.com/p/17AHl
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize.
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize.Picha: Getty Images

Wasiwasi umezidi kutanda nchini humo wakati muungano wa waasi hao unaojulikana kama Seleka ukizidi kusonga mbele kuelekea mji mkuu Bangui, kwa madai kuwa serikali imekiuka makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2007. Lakini rais Francois Hollande wa Ufaransa amekataa ombi la rais Francois Bozize akisema kuwa muda wa kufanya hivyo ulikwisha.

Wakaazi wa Bangui wakiandamana kuishinikiza Ufaransa kuchukua hatua dhidi ya waasi wa Seleka.
Wakaazi wa Bangui wakiandamana kuishinikiza Ufaransa kuchukua hatua dhidi ya waasi wa Seleka.Picha: Reuters

Marekani yaamua kufunga ubalozi wake

Marekani kwa upande wake imetangaza jana Alhamisi kuwa inasitisha shughuli zote katika ubalozi wake mjini Bangui, na kwamba balozi wake na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo walikuwa wameondoka nchini humo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Patrick Ventrell, alisema uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi hao, na kwamba hatua hiyo haihusiani kwa namna yoyote ile na uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili. Marekani pia iliwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hayo yanajiri wakati viongozi wa kanda hiyo wakijaribu kuratibu makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi walikuwa wamesema wamesimamisha kwa muda, operesheni kuelekea mji mkuu, ili kuruhusu mazungumzo kufanyika. Waasi hao wanataka serikali itekeleze makubaliano ya kuwatawanya na kuwaingiza katika maisha ya kiraia.

"Wapiganaji wanataka pesa walizoahidiwa ili kuweza kujiunga na jamii ya kiraia, programu ya kuwatawanya ilihusu kuwanyang'anya silaha wapiganaji lakini yote hayo hayakutekelezwa na ndiyo matatizo makubwa. Lingine ni kuundwa kwa ajira kwa waasi kwa lengo la kuwaingiza katika maisha ya kiraia," alisema Thierry Vircoulon kutoka shirika la kutatua migogoro la International Crisis Group, anafafanua madai ya waasi hao.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande.Picha: AFP/Getty Images

Seleka waapa kumuangusha Bozize

Muungano huo wa Seleka umeapa kumuangusha Bozize kama hatatekeleza makubaliano yaliyopita kwa ukamilifu. Lakini Bozize anataka waasi hao wasimamishwe kwanza ili kufanikisha mazungumzo, ambayo viongozi wa kanda wanasema yanaweza kufanyika katika mji mkuu wa Gabon, Libreville.

Ufaransa ina wanajeshi 250 katika koloni lake hilo la zamani, ambao ni sehemu ya walinda amani, na utawala mjini Paris umefanya juhudi za kila aina huko nyuma kumlinda rais Bozize dhidi ya waasi mwaka 2006. Lakini rais Francois Hollande alisema kama nchi yake ina wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya kati, basi wanajeshi hao ni kwa ajili ya kulinda raia wa Ufaransa na maslahi ya nchi hiyo, lakini si kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Waasi wauzingira mji mkuu Bangui

Kuna raia wa Ufaransa wapatao 1,200 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wengi wao wakiwa mjini Bangui, ambako wanafanya kazi na makampuni ya uchimbaji madini na mashirika ya misaada, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa. Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Ulaya lililopo nchini humo halijaonyesha dalili zozote za kuchukua upande katika mgogoro huo. Nchi jirani ya Chad imetuma wanajeshi 150 kujaribu kupambana na waasi hao.

Ubalozi wa Ufaransa mjini Bangui.
Ubalozi wa Ufaransa mjini Bangui.Picha: Reuters

Ahadi za huko nyuma kwa waasi zilivunjwa na chanzo kimoja cha kidiplomasia kilisema waasi wamechukua maeneo kuuzunguka mji wa Bangui siku ya Alhamisi, na hivyo kuuzingira kabisaa. Hali iliendelea kuwa ya wasi wasi katika mji huo mkuu, siku moja baada ya kutokea maandamano, na wakaazi walianza kuhifadhi maji na vyakula. Bozize aliingia madarakni mwaka 2003 kupitia uasi uliomuondoa rais Ange-Felix Patasse.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo