1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yafuzu fainali za Ligi ya Mataifa ya UEFA

Bruce Amani
16 Novemba 2020

Wakati mashindano ya kimataifa ya mwaka huu yakifikia kikomo, wachezaji hawana muda wa kupumzika kwasababu ligi za kitaifa zinarudi kwa kasi wikiendi ijayo.

https://p.dw.com/p/3lN0Y
UEFA Nations League | Portugal vs. Frankreich | Jubel Frankreich
Picha: Rafael Marchante/REUTERS

Ufaransa ndiyo taifa pekee lililojihakikishia nafasi katika fainali za Ligi ya Mataifa na itaialika Sweden kesho. Hii ni baada ya kupata ushindi wa nadra wa 1 – 0 dhidi ya Ureno mwishoni mwa wiki matokeo ambayo yalimridhisha kocha Didier Deschamps. "Kuwa na mchezo kama huu tuliocheza unadhihirisha ubora wa kiwango cha timu ya Ufaransa, uwezo wetu wa kujitokeza katika mechi zenye ushindani mkubwa na kuonyesha kandanda safi la kiufundi. Na dhidi ya mpinzani kama huyu, ni fahari kubwa sana kwangu kuwaona wachezaji wakicheza kwa njia hii."

Nafasi tatu bado zipo wazi na Ujerumani itahitaji tu sare dhidi ya Uhispania ugenini kesho ili kutinga hatua ya mwisho ya mashindano hayo. Hii ni baada ya kuizaba Ukraine 3 – 1 Jumamosi. Uhispania ilitoka sare ya 1 – 1 na Uswisi.

Katika Kundi A1 Italia itakuwa mgeni wa Bosnia and Herzegovina, ambao hawawezi tena kufika katika fainali hizo, wakati Poland itaialika Uholanzi Jumatano. Katika siku hiyo Ubelgiji itacheza dhidi ya Denmark katika mtanange mwingine wa kuwania nafasi ya kwanza ya kundi A2 wakati England, ambao tayari wameondolewa, wakiwakaribisha Iceland. England walifungwa jana 2 – 0 na Ubelgiji. 

Afp, ap, reuters, dpa