1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa: Sera za Sarkozy zinalipizwa kisasi

Maja Dreyer28 Novemba 2007

Kwa usiku wa tatu mfululizo, vijana katika vitongoji vya mji mkuu Paris nchini Ufaransa wameendelea kufanya machafuko. Hiyo ni moja kati ya masuala yanayozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii.

https://p.dw.com/p/CU6b
Polisi inapiga doria katika vitongoji vya Paris
Polisi inapiga doria katika vitongoji vya ParisPicha: AP

Kwanza ni gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin ambalo limeandika hivi:


“Alipokuwa badi waziri wa mambo ya ndani, Nicolas Sarkozy aliahidi kuwaondosha wahuni hao. Lakini tangu kuingia katika cheo cha urais, inaonekana kama ana malengo mengine. Badala ya kushughulikia matatizo katika vitongoji, kwanza, rais huyu alipunguza kodi kwa matajiri. Aliongeza muda wa kufanya kazi, aliiwekea mipaka haki ya kufanya maandamano na kuongeza michango ya wananchi kwa bima ya afya. Sera hizo zinazowaathiri walio maskini zinalipizwa kisasi katika mitaa hiyo ya Paris hata kwa chuki zaidi kuliko miaka miwili iliyopita.”


Mhariri wa gazeti la “Fränkischer Tag” anamwunga mkono mwenzake wa “Tageszeitung” na anaongeza kusema:


“Rais Sarkozy, tangu kuingia madarakani, hajawatembelea watu kwenye mitaa maskini ambao anawaona kuwa kama takataka. Juu ya hayo aliweka sheria mpya inayotaka jamaa wa wahamiaji waliokwenda Ufaransa wafanye vipimo vya jenetiki ili kutoa ushahidi kuwa kweli ni ndugu. Kwa hivyo, si jambo linaloshangaza kwamba wakaazi wa vitongoji wa mjini Paris wanachukia chochote kinachowakilisha serikali, ikiwa ni rais au polisi. Kwao ni kama maadui na wameanzisha vita.”


La mwisho juu ya suala hilo tunasikia uchambuzi wa gazeti la “Frankfurter Neue Presse” ambalo linalinganisha hali ya wahamiaji nchini Ufaransa na ile ya hapa Ujermani. Limeandika:

“Zaidi kuliko nchini Ujerumani, Ufaransa kwa miaka mingi ilishindwa kufahamu matokeo ya uhamiaji usiodhibitiwa. Kwa kipindi kirefu, wahamiaji hawakusaidiwa. Sasa kizazi kizima kimepotea. Inabidi kutofanya kosa hilo hilo tena. Ikiwa elimu kwa watoto wa wahamiaji haiimarishwi, basi pamoja na kusababisha hali ngumu katika familia husika pia nchi inapoteza uwezo mkubwa wa kibindamu. Na juu ya hayo sera hizo mbaya ni msingi wa machafuko tunayoweza kuyaona siku hizi kwa mara nyingine tena.”

Tubadili mada na kuelekea Annapolis. Mhariri wa “Thüringer Zeitung” ameshtushwa na sentensi moja ya Rais Bush ambayo ni hii:


“Vita kuhusu mustakabali wa Mashariki ya Kati vimeanza. Hivyo ndivyo alivyosema rais Bush. Kweli vita? Je, lengo la mkutano wa Annapolis si kuzungumzia amani? Haipaswi kutumia lugha ya kijeshi tena. Lakini lengo la rais Bush kufanya mkutano huu ni wazi, anataka kudhoofisha mamlaka ya Iran katika eneo hili. Tena namna serikali ya Iran inavyokasirika inaonyesha kwamba Bush aligusa suala tete. Ndivyo vita hivyo Bush alivizungumzia. Bado analigawa eneo la Mashariki ya Kati katika pande mbili, zuri na baya.”