1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Washirika wake waamua kuondoka Mali

Grace Kabogo
17 Februari 2022

Ufaransa na washirika wake wa Ulaya wanaoshiriki katika operesheni dhidi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali wameamua kuondoa vikosi vyao na rasilimali nyingine za kijeshi.

https://p.dw.com/p/479zh
Mali Frankreich beendet die Operation „Barkhane“
Picha: AP Photo/picture alliance

Lakini katika tangazo lao la pamoja, nchi hizo zimekubaliano juu ya mipango ya kusalia katika ukanda wa Sahel, hususan nchini Niger na katika Ghuba ya Guinea hadi Juni mwaka huu.

Uhusiano baina ya Ufaransa na Mali umevurugika tangu watawala wa kijeshi wa Mali walipoahirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi huu wa Februari, hadi mwaka 2025.

Watawala hao pia wamezikasirisha nchi za Ulaya kwa kufanya mkataba na kampuni binafsi ya kiulinzi kutoka Urusi, ambayo nchi hizo zinasema haiendani na maadili ya operesheni yao.

Nchi 14 za Ulaya zinajumuishwa katika operesheni za kijeshi za Barkhane na Takuba za kupambana na ugaidi katika ukanda wa Sahel.