1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufadhili zaidi,dawa na unyanyapaa wajadiliwa Mexico

Kitojo, Sekione4 Agosti 2008

Mkutano wa dunia kuhusu ukimwi unaendelea leo Jumatatu baada ya kuelezwa kuwa ushindi dhidi ya ugonjwa huo uko mbali.

https://p.dw.com/p/Eq9T
Wajumbe katika mkutano wa 17 wa Ukimwi huko MexicoPicha: AP


Mkutano wa dunia kuhusu ukimwi unaendelea leo Jumatatu baada ya kuelezwa kuwa ushindi dhidi ya ugonjwa huo uko mbali na watu waliokatika hatari wanaweza kunusurika iwapo zitapatikana fedha zaidi. Hiyo ni baada ya kutolewa miito jana Jumapili wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mjini Mexico City kuwa dunia haipaswi kuacha kupambana na ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 25 hadi sasa.

Upatikanaji wa fedha zaidi, upatikanaji wa matibabu, kuongeza nguvu ya uzuiaji wa virusi vinavyoharibu kinga ya mwili HIV, pamoja na uovu wa kijamii unaotokana na matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake ni masuala muhimu katika mkutano huo wa siku sita.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon , katika ufunguzi wa mkutano huo siku ya Jumapili , ameyataka mataifa fadhili kutekeleza majukumu yao yaliyopitishwa katika mkutano wa umoja wa mataifa na mkutano wa kundi la mataifa tajiri yenye viwanda G8 ili kufanikisha hatua ya kupatikana kwa msaada wa madawa dhidi ya HIV na ukimwi ifikapo mwaka 2010.


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameongeza kuwa wakati mapambano dhidi ya ukimwi yanakaribia kumaliza muongo wa tatu, bado tunakabiliwa na upungufu mkubwa katika uwezo wa kupambana nao.

Mapambano dhidi ya ukimwi na HIV yanahitaji upatikana wa fedha wa muda mrefu na endelevu. Wakati watu zaidi wanapata matibabu na kuishi kwa muda mrefu zaidi, fedha zaidi zinapaswa kuongezwa katika muda wa miongo michache ijayo. Katika mataifa yaliyoathirika zaidi, wafadhili wanapaswa kutoa fedha zaidi.

Zaidi ya watu milioni 25 wamekufa kutokana na ugonjwa huo wa ukimwi tangu kuzuka kwake mara ya kwanza 1981 na watu milioni 33 hadi sasa wanaishi na virusi vya HIV. Asilimia 90 ya wale walioathirika wako katika mataifa masikini. Katika miaka miwili iliyopita , kumekuwa na msaada mkubwa kwa watu hawa , lakini hata hivi sasa , ni watu milioni tatu tu, ama pungufu ya theluthi ya watu wenye mahitaji , wanapata matibabu ya madawa ya kurefusha maisha.

Margaret Chan mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la umoja wa mataifa WHO , ameonya kuwa vita dhidi ya ukimwi vitakuwa virefu.

Mkutano huo wa kimataifa wa siku sita ni wa kwanza kufanyika katika Latin Amerika , eneo ambalo limekumbwa na doa la kuwatenga watu wanaoishi na virusi vya HIV.

Zaidi ya wanasayansi, wanasiasa na wafanyakazi wa kupambana na ukimwi 22,000 wanahudhuria mkutano huo , ukiwa ni mkutano mkubwa kabisa katika historia ya miaka 27 ya ugonjwa huo, na mkubwa kabisa kufanyika katika nchi inayoendelea.

Peter Piot, mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa mataifa la kupambana na ukimwi UNAIAS ameusifu mkutano huo kuwa ni sababu kubwa ya kutia moyo. Ameongeza kuwa ni mapema mno kusema tumeshinda , kwasababu mafanikio ya kuushinda ukimwi hayako karibu.

Watafiti kutoka Uswisi hata hivyo walishangiliwa katika mkutano huo , lakini pia walikabiliwa na maswali mengi jana Jumapili wakati walipoeleza kuwa wagonjwa wenye virusi vya HIV ambao wanapata matibabu ya dawa za kurefusha maisha hawawezi kuambukiza virusi hivyo wakati wa kufanya ngono bila kutumia mipira. Maelezo yao katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa mkutano huo yamepingwa na baadhi ya wajumbe, ambao wanahofia kuwa inaweza kuleta hisia kuwa watu wanaweza kufanya mapenzi bila kutumia kinga.