1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti

Sekione Kitojo5 Julai 2010

Mada mbili zimewashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo, mchezo ulioonyeshwa na timu ya Ujerumani katika kombe la dunua na kura ya maoni kuwalinda wasiovuta sigara huko Bavaria.

https://p.dw.com/p/OAu1
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikuwapo uwanjani akiwashuhudia vijana wa Joachim Löew wakiwachezesha dansi ya tango vijana wa Maradona, Argentina.Picha: picture-alliance/dpa

Udondozi wa maoni yaliyoandikwa katika magazeti ya hapa Ujerumani, mada mbili zilizowashughulisha zaidi wahariri wa magazeti hii leo, ni pamoja na mchezo ulioonyeshwa na kikosi cha Ujerumani katika fainali za kombe la dunia huko Afrika kusini , na kura ya maoni iliyokusudia kuwalinda wasiovuta sigara katika jimbo la kusini nchini Ujerumani la Bavaria.

Tukianza na gazeti la Volksstimme la Magdenburg, linaandika kuhusu fainali za kombe la dunia zinazoendelea huko Afrika kusini. Gazeti linaandika.

Ghafla kikosi cha Ujerumani kimekuwa kipenzi cha wapenda soka duniani. Aina ya kandanda inayoonyeshwa na kikosi hicho, inakumbusha enzi za kina Becknbauer na Günter Netzer katika mwaka 1972. Kama vijana wa Joachim Löew walivyowachezesha Tango vijana wa Maradona na Messi, imewashangaza hata baadhi ya wataalamu. Kutokana na aina ya mchezo waliyouonyesha ,wenye lengo, ubunifu, na mbinu , ni kandanda safi, ambalo linaweza kuitwa "la kimapenzi".

Ni kweli kwamba Ujerumani ambayo hupendelea zaidi mpira wa kimbinu, haikuwa katika zile timu za juu kabisa. Lakini mipango na malengo sahihi, pamoja na uwezo wa kimwili, na mchezo wa kitimu, vimekifanya kikosi hiki, kuwa mbele ya timu nyingine kubwa za dunia. Si bure kwamba , wachezaji maarufu duniani kama Messi, Kaka, Ronaldo na Rooney wanaangalia mashindano haya kwa mbali hivi sasa.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten, likizungumzia kuhusu mada hiyo linaandika.

Kandanda ndio burudani kuu hivi sasa duniani, Ujerumani hivi sasa imejitokeza mbele. Kama vijana wa Joachim Löew walivyoweza kuushangaza ulimwengu wa kandanda, ndivyo watu katika nchi hii pia walivyojawa na shauku. Kiongozi ambaye anajua anataka kufanya nini pamoja na timu inayojitolea kwa uwezo wao wote bila ya kufanya makosa na kiburi.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung, linalochapishwa huko Lüneburg, anampiga vijembe kansela wa Ujerumani Angela Merkel kutokana na mchezo walionyesha vijana wa Ujerumani katika kombe la dunia.

Binafsi kansela Merkel alikuwapo uwanjani, wakati Ujerumani ikiwapeleka puta Waargentina. Merkel alipata somo kutokana na kandanda safi, utendaji wa pamoja wa timu na nia ya timu. Na uzoefu alioupata ni kwamba , ni jinsi gani vijana hawa wamekuwa mabalozi wazuri wa nchi yake, wakati yeye binafsi alionekana akitabasamu wakati wote wa mchezo. Hakuna mtu ambaye atataka kuiga tabasamu hilo katika chama cha kansela Merkel , pamoja na mshirika wao chama cha FDP. Lakini wanatakiwa kwa pamoja kufanyakazi na kusonga mbele, kama walivyofanya kina Schweini, Poldi na wenzao, na hayo ndio matamanio ya watu katika nchi hii. Ujerumani ni mabingwa wa dunia wa kusafirisha bidhaa nje, ni mabingwa wa dunia katika utalii, na pia inaelekea tunaweza kuwa mabingwa wa dunia katika kandanda.

Tukibadilisha mada, gazeti la Abendzeitung la mjini Munich linaandika kuhusu uamuzi wa umma kuhusu marufuku ya kuvuta sigara. Gazeti linaandika.

Kutokana na suala moja, watu wote wa Bayern tunaweza kufurahia. Hatimaye, mjadala unaosumbua jimbo zima na ulioendesha kijazba, umefika mwisho. Wananchi wameufikisha mwisho, ambapo serikali ya jimbo kwa muda wa miaka kadha haikuweza kuutatua, kwa kuweka sheria ya wazi ya kuwalinda wale wasiovuta. Zaidi ya wapiga kura asilimia 60 wametoa uamuzi wao kutaka sheria kali dhidi ya uvutaji sigara. Licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wavutaji, wakisaidiwa na makampuni yanayouza tumbaku.

Gazeti la Saarbrücker Zeitung, kuhusu uamuzi wa kupiga marufuku uvutaji sigara katika jimbo la Bavaria , linaandika.

Mtu anatambua , kuwa uamuzi wa wananchi huko Bayern unapaswa kupongezwa. Mara hii watawaliwa nao wamechukua nafasi yao , mbali ya kundi lililo na ushawishi la viwanda na wauzaji wa tumbaku, pamoja na wakulima. Licha ya makampuni ya tumbaku na mikahawa kuwekwa ukutani, nchi nzima , pamoja na hata Austria walikuwa wakikodolea macho yao katika kura hiyo ya maoni huko Bayern. Hivi sasa ishara inayotoka huko Munich, ni kwamba idadi kubwa ya wapiga kura wametoa ujumbe wa wazi kuwa matamanio yao ni kulindwa kwa wale wasiovuta sigara.

Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse

Mhariri: Mwadzaya,Thelma