1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UDONDOZI WA MAGAZETI

Erasto Mbwana18 Mei 2006

Maoni ya Wahariri wengi wa magazeti ya Ujerumani yaliyotoka leo asubuhi yamejishughulisha zaidi na uamuzi wa serikali ya Ujerumani wa kupeleka Wanajeshi 800 wa Kijerumani watakaolinda amani wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia utakaofanywa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwishoni mwa mwezi wa Julai mwaka huu. Mada nyingine iliyodondolewa ni onyo la aliyekuwa Msemaji wa serikali, Uwe-Karsten Heye kuwa Waafrika, wakati wa michuano ya kombe la dunia la kandanda, waepuke kwenda Brandenburg kwa sababu ya uhasama dhidi ya Wageni.

https://p.dw.com/p/CHW4

“ABENDZEITUNG” likijishughulisha na uamuzi wa serikali ya Ujerumani wa kupeleka Wanajeshi 800 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limeandika:

“Ujerumani na nchi za Umoja wa Ulaya zinapaswa kusaidia kwa dhati na kuunga mkono uchaguzi huru wa Kongo-Kinshasa. Safari hii kinachohusika zaidi siyo mafuta au kupambana na ugaidi isipokuwa kuisaidia nchi hiyo iwe na amani, demokrasia na uimara. Isitoshe, huo utakuwa ujumbe wa kwanza wa kijeshi chini ya uongozi wa Ujerumani. Isingaliwezekana hata kidogo miaka 20 iliyopita kwa Ujerumani kupewa jukumu kama hilo katika nchi za nje. Lakini siku hizi hakuna anayelalamika tena ndani na hata nje ya Ujerumani. Hili limekuwa jambo la kawaida na ni ishara nzuri.”

Hayo yalikuwa maoni ya “ABENDZEITUNG.”

SCHWERINER ZEITUNG” likiunga mkono uamuzi huo na kutilia mkazo limeandika:

“Kikosi hicho cha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni huduma ya kidiplomasia. Ingawaje Wakosoaji wengi wa kisiasa wana wasiwasi na ujumbe huo lakini hawakosoi kikosi chenyewe isipokuwa matayarisho yake na idadi yake. Wakosoaji wana wasiwasi kuwa ikiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vitazuka, Wanajeshi hao watalazimika kukaa kwa muda mrefu badala ya miezi minne kama ilivyopangwa. Lakini kwa upande mwingine ni muhimu zaidi kuona kuwa uchaguzi, unaofanywa baada ya miaka 40, unakuwa huru na wa kidemokrasia. Lazima fursa hiyo itumiwe vizuri.”

Maoni ya SCHWERINER ZEITUNG.”

Gazeti la „FRANKFURTER RUNDSCHAU“ likiwa na mashaka limeandika:

„Kinachokosolewa hapa ni vile jinsi Wanasiasa wa nchi hii wanavyochukua uamuzi wakati mwingine. Tunaunga mkono juhudi za kuona kuwa uchaguzi utakuwa wa amani na Kongo-Kinshasa inakuwa imara, ina utulivu na demokrasia. Lakini ingawaje ni hivyo, ujumbe huo umetayarishwa vibaya na idadi ya Wanajeshi watakaopelekwa huko ni ndogo sana. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuwa na uchaguzi ulio huru na wa kidemokrasia kutategemea sana kuwako kwa amani kila mahali. Isitoshe, hakuna uthibitisho wowote ule kuwa katika muda wa miezi hiyo minne utulivu utaendelea kuwapo,“

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la „FRANKFURTER RUNDSCHAU.“

Gazeti la „NEUE DEUTSCHLAND“ likikosoa vikali limeandika:

„Watu wanapaswa kuwatazama Wakongo machoni mwao vile jinsi watakavyowapokea Wanajeshi hao. Yote hayo yatakwisha wakati Wanajeshi, waliopata mafunzo bora, watakapoanza kupambana na mtoto mwenye kalashinikov. Hawatafikiri tena. Hicho ndicho ambacho Waziri wa Ulinzi, Jung na Majemadari wake, wanachojaribu kuzuia. Ndiyo maana, Wanajeshi hao watawekwa mjini Kinshasa peke yake. Lakini swali linalopaswa kuulizwa hapa ni hili: Je, itatokea nini iwapo Wanajeshi hao watashambuliwa? Majukumu yao hayawezi kujibu swali hili na wala haijulikani ni umbali gani wanaoweza kwenda nje ya Kinshasa wakati mashambulio yatakapotokea.“

Maoni ya gazeti la „NEUE DEUTSCHLAND.“

Gazeti la „MANNHEIMER MORGEN“ likiunga mkono onyo la aliyekuwa Msemaji wa serikali, Uwe-Karsten Heye kuwa Waafrika, wakati wa michuano ya kombe la dunia la kandanda, waepuke kwenda Brandenburg kwa sababu ya uhasama dhidi ya wageni limeandika:

„Siyo jambo la kushangaza hata kidogo kuona kuwa Viongozi wa misafara ya kimataifa na Shirikisho la vyama vya Afrika nchini Ujerumani wamechapisha orodha ya miji iliyoko mashariki mwa Ujerumani inayopaswa kuepukwa. Wanasiasa wa miji inayohusika wanapinga vikali onyo hilo. Lakini kushambuliwa kwa Mjerumani mwenye asili ya Kiafrika, Ermyas M, mjini Potsdam ni ushahidi wa kutosha wa jinsi hali halisi ilivyo. Michuano ya kombe la dunia, kwa mara nyingine tena, inaipa fursa ya mwisho Ujerumani, kama mwenyeji, kuboresha haiba yake ikiwa vitendo viovu dhidi ya Wageni havitatokea.“

Hayo yalikuwa maoni ya gazeti la „MANNHEIMER MORGEN.“

„MÄRKISCHEN ODERZEITUNG“ likiwa na maoni tofauti kabisa limeandika:

„Ni kweli kabisa kwamba kuna Wanamgambo wa Kinazi mambo leo, kuna uhasama dhidi ya Wageni na kuna wenye itikadi kali za mrengo wa kulia. Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha katiba ya Wizara ya Sheria inasema kuwa kuna Manazi mambo leo 1,385 kati ya wakazi wote zaidi ya millioni mbili na nusu. Ndiyo, Brandenburg imefungua macho ya Walimwengu. Lakini siyo haki hata kidogo kwa kile kilichotokea kuwapaka matope Wabrandenburg wote. Wakazi wa mkoa huo wanapaswa kuelemishwa jinsi ya kushirikiana na wageni na kuheshimu maoni ya watu wengine.“

Kwa maoni hayo ya „MÄRKISCHEN ODERZEITUNG“ kuhusu onyo la aliyekuwa Msemaji wa serikali, Uwe-Karsten Heye kuwa Waafrika, wakati wa michuano ya kombe la dunia la kandanda, waepuke kwenda Brandenburg kwa sababu ya uhasama dhidi ya Wageni ndiyo yote tuliyoweza kuwachambulia kutoka magazeti ya Ujerumani.