Uchumi imara na wa mafanikio | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 10.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Uchumi imara na wa mafanikio

Ujerumani imeweza kupitia katika msukosuko wa uchumi bila ya kukwaruzika hata kidogo, lakini kila upande, wa serikali na wa upinzani, unadai kuwa ndio ulioyaleta mafanikio hayo.

"Nawashukuru kwa yale mliyoyafanya kwa ajili ya nchi yetu" Na pia nawashukuru kwa yale mnayoyafanya kwa ajili ya Ulaya." Hayo aliyasema Kansela Angela Merkel kwa wajasiriamali mnamo mwezi wa Juni mwaka huu.

Angela Merkel hakutaka kumwachia mtu mwengine kuzitoa shukrani hizo kwa mameneja katika siku ya "viwanda vya Ujerumani" kwani sekta ya viwanda inatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba hata katika nyakati za migogoro , Ujerumani inaikabili migogoro hiyo vizuri.

Katika hilo, kila upande, unataka kujipatia sifa- ule wa serikali na ule wa upinzani kadhalika. Theluthi moja ya tija ya uchumi nchini Ujerumani inatokana na mchango unaotolewa na sekta ya viwanda. Sekta hiyo inatoa ajira kwa watu milioni nane nchini Ujerumani.

Ni kutokana na mafanikio hayo kwamba Rais wa Baraza la Viwanda nchini Ujerumani (BDI) Ulrich Grillo ameiita sekta ya viwanda kuwa ni mashine ya kuzalisha nafasi za ajira.

Bidhaa za Ujerumani zatakiwa duniani kote

Kansela Angela Merkel (kushoto), Waziri wa Uchumi Phillip Rösler na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang.

Kansela Angela Merkel (kushoto), Waziri wa Uchumi Phillip Rösler na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang.

Hakuna nchi nyingine yoyote duniani yenye viwanda vya ukubwa wa kati vinavyomilikiwa na familia za wajasiramali, vilivyofanikiwa kama Ujerumani. Viwanda vinavyohesabika kuwa na ukubwa wa kati nchini Ujerumani ni pamoja vile vyenye wafanyakazi 500.

Na katika kila viwanda vitano nchini Ujerumani vinne vinamilikiwa na familia. Bidhaa zinazozalishwa Ujerumani, zinatakiwa duniani kote hadi leo na hasa katika nchi zinazoinukia zenye unomi wa kiuchumi: magari, mashine na bidhaa za kikemia.

Robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje zinatoka katika viwanda vyenye ubunifu wa hali ya juu. Asilimia 90 ya bajeti inayotengwa kwa ajili ya utafiti na maendeleo nchini Ujerumani inakwenda katika viwanda. Nchi nyingine za Ulaya kwa wastani zinafikia asilimia 70 tu.

Ujerumani leo imefikia ilipo katika mafanikio kwa sababu maendeleo ya viwanda yalianza miaka zaidi 150 iliyopita. Sekta ya viwanda itaendelea kuwa msingi wa uchumi nchini Ujerumani.

Bara la Ulaya linakuwa na udhaifu pale ambapo sekta ya viwanda haitoi mchango.

Mwenyekiti wa Baraza la Viwanda nchini Ujerumani, Bwana Grollo, amesema sekta dhifu ya viwanda maana yake kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira na pia maana yake ni kuyumba kwa jamii. Na kweli Ujerumani ndiyo nchi yenye sekta kubwa kabisa ya viwanda barani Ulaya.

Kujikwaa si kuanguka

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble.

Kutokana na mgogoro wa fedha,ustawi nchini Ujerumani ulishuka kwa asilimia 5 mnamo mwajka wa 2009.Lakini baada ya miaka miwili tu kiwango cha hapo awali kilifikiwa.Lakini hali hiyo haikuwa rahisi, kwani mwanzoni mwa Milenia Ujerumani ilipewa jina la " mgonjwa wa barani Ulaya"

Mnamo mwaka wa 1998 vyama vya SPD na Kijani viliingia serikalini na ziliuanzisha mpango wa mageuzi ulioitwa "Ajenda 2010. Soko la ajira na mfumo wa kijamii ulifanyiwa ukarabati.Mnamo mwaka wa 2007, serikali ya mseto ya vyama vya CDU,CSU na SPD viliuendeleza mpango huo, ikiwa pamoja na utaratibu wa kustaafu kuanzia umri wa miaka 67, badala ya umri wa miaka 67.

Kansela Angela Merkel amesema Ujerumani leo imo katika hali nzuri sana kutokana na mageuzi yaliyofanywa katika soko la ajira na katika mfumo wa bima za kijamii. Mtaalamu wa masuala ya kijamii Bert Rüpp amesema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Ujerumani imejijenga upya kiuchumi.

Mgogoro wa fedha

Mgombea wa kiti cha ukansela kwa tiketi ya SPD, Peer Steinbrück.

Mgombea wa kiti cha ukansela kwa tiketi ya SPD, Peer Steinbrück.

Hata hivyo, tokea kufumuka kwa mgogoro wa fedha na wa kiuchumi ulioandamana na madeni mtazamo wa kimegeuzi umelegea kidogo nchini Ujerumani. Kilichokuwa kinafanyika ni kujaribu kuyapunguza makali ya athari za mgogoro. Lakini juhudi hizo ziliiwezesha Ujerumani kuponyoka bila hata ya mkwaruzo.

Je, hali itakuwaje katika siku za usoni nchini Ujerumani? Mnamo miaka ya 90 masuala muhimu yalikuwa gharama za mishahara, mzigo wa kodi na urasimu. Suala la urasimu bado linaendelea Lakini mazungumzo juu ya kodi na mishahara yamepungua .

Mgombea ukansela wa chama cha SPD, Peer Steinbrück, anataka kuanzishwa utaratibu wa mshahara wa kima chini kwa wote wa Euro 8.50 kwa saa. Lakini Kansela Merkel analipinga wazo hilo. Uhaba wa wafanyakazi wenye ustadi, ugeugeu wa bei za malighafi na suala la nishati ni mambo yatakayoendelea kuikabili Ujerumani katika siku za usoni hata baada ya uchaguzi.

Mwandishi: Sabine Kinkartz
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com