Uchambuzi wa wahariri wa Ujerumani | Magazetini | DW | 13.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa wahariri wa Ujerumani

Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Mkuu wa shirika la Telekom la Ujerumani,Kai-Uwe Ricke amejiuzulu baada ya miaka mine madarakani.Nafasi yake itashikiliwa na mkuu wa tawi la simu za mkono-T-Mobile,René Obermann.Mageuzi katika uongozi wa shirika hilo kubwa kabisa la mawasiliano ya simu barani Ulaya ndio mada kuu iliyogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani hii leo.Lakini hata mkutano mkuu wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia-NPD umemulikwa na wahariri wa humu nchini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaandika:

„Amekawia sana mkuu wa shirika la Telekom kushughulikia kishindo kilichosababishwa na mashindano makubwa ya kibiashara nchini Ujerumani.Katika wakati ambapo mashirika mengine yamekua yakiwanasa watu kwa malipo nafuu kwa huduma jumla za mawasiliano ya simu na mtandao wa Internet na kujibwaga katika soko la bei za chini kabisa za simu za mikono-shirika la Telekomo limepoteza matawi yake katika mashindano hayo ya kibiashara.René Obermann,kiongozi mpya wa Telekom- shirika kubwa kabisa la mawasiliano ya simu barani Ulaya,hatakua na kazi rahisi.

Gazeti la KÖLNER STADT-ANZEIGER linaitwika pia serikali kuu ya Ujerumani jukumu la mizozo ya shirika la Telekom:Gazeti linachambua:

„Suala hapa ni kama kiongozi mpya wa Telekom,René Obermann atafanikiwa kusitisha mmomonyoko katika mfumo asilia wa mawasiliano ya simu.Kuzuwia wimbi la watu wanaolipa kisogo shirika hilo si jambo linalowezekana- na pengine serikali kuu na taasisi ya shirikisho inayoshughulikia mawasiliano ya simu ndivyo walivyokua wakitaka hivyo.Kwasababu tangu mwanzo shabaha ya serikali kuu ilikua kuacha kudhibiti peke yake shirika hilo na kulibinafsisha.Kwa hivyo ni jambo la kustaajabisha kuona hii leo serikali kuu inajiuliza kwanini shirika hilo limebanwa.

Gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG la mjini Düsseldorf linahisi:

„Hata kama René Obermann anaetazamiwa kushika nafasi ya Ricke,anatajikana kua mtaalam mwenye hima,na asiyekua na shida,hata hivyo atahitaji maguvu na bahati pia.Mapambano ya kuania wateja yatakua makali zaidi hivi sasa katika soko lililobadilika,seuze tena serikali kuu imepunguza tena kiwango cha hisa zake zinazofikia asili mia 33.Kila mteja mpya,naiwe wale wanaolaumiwa na kuitwa „nzige“ au wengineo,atataka tuu kuona tija inapatikana haraka na thamani na faida ya hisa za Telekom zinapanda.“

Mada nyengine magazetini inahusu chama cha siasa kali za mrengo wa kulia NPD ambacho wafuasi wake wameitisha kwa madoido mkutano wao mkuu mwishoni mwa wiki hii mjini Berlin.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na kupima hoja zinazozushwa tena kutaka chama hicho cha chuki dhidi ya wageni kipigwe marufuku.