1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin7 Machi 2007

Maafisa wanaopelekwa kufanya kazi katika miji mikubwa,hawana haki ya kudai nyongeza ya mishahara.

https://p.dw.com/p/CHTY

Uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba ya Ujerumani umegonga vichwa vya habari katika magazeti mengi ya leo hii nchini Ujerumani.Mada nyingine ni operesheni mpya ya vikosi vya NATO nchini Afghanistan.

Tunaanza na gazeti la BADISCHE TAGBLATT linalokosoa uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya Ujerumani kutupilia mbali ombi la afisa wa polisi aliehamishwa kufanya kazi katika jiji la Munich. Yeye,amedai nyongeza ya mshahara kwa sababu ya gharama kubwa za kuishi katika jiji kubwa kulinganishwa na sehemu za mashambani. Gazeti hilo linasema:

Wale wanaopaza sauti kuhusu haja ya kuwepo usalama wa umma,ndio hupaswa kuhakikisha kwamba walinzi wa usalama wanaweza kutekeleza kazi zao katika hali ya kiuchumi inayoweza kuhalalishwa. Wanasiasa bila shaka watalizingatia suala hilo kwa sababu wapaswa kufanya hivyo.“

Na kwa maoni ya gazeti la MANNHEIMER MORGEN:

“Uamuzi uliopitishwa na Mahakama ya Katiba ya Ujerumani,ni ushahidi mpya kuwa kuna haja kubwa ya kufanywa mageuzi ya kisheria kuhusu masharti ya ajira.Kwani pendekezo lililotolewa na waziri mkuu wa jimbo la Baden-Württemberg,bwana Günther Oettinger kuwapa nyongeza maafisa wanaofanya kazi katika miji mikubwa,halikuwekewa vipangamizi na Mahakama ya Katiba.Lakini pendekezo hilo halitopokewa kwa furaha na mashirika ya binafsi katika sekta ya uchumi.

Sasa tutupie jicho mada nyingine iliyogonga vichwa vya habari-nayo ni operesheni mpya ya vikosi vya NATO,kusini mwa Afghanistan iliyopewa jina la shujaa wa Kigiriki “Achilles.“ Vikosi vya NATO vikishirikiana na majeshi ya Afghanistan, vinapigana na Wataliban na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya kusini mwa nchi.

Kwa maoni ya gazeti la LANDESZEITUNG: “Nguvu za kijeshi peke yake,hazitoleta utulivu katika nchi hiyo iliyoteketezwa kwa vita.Operesheni ya kijeshi inapaswa kwenda sambamba na miradi ya kuwasaidia raia.Kwa upande mwingine picha za raia waliouawa kwa makosa,huenda zikatumiwa na Wataliban kama silaha,dhidi ya vikosi vya NATO.

Na gazeti la WESER-KURIER linasema operesheni ya NATO ni barabara.Likiendelea linaeleza hivi:

Hatimae vikosi vya NATO vinachukua hatua ya kuwapiga vita Wataliban.Hiyo ni njia pekee ya kupunguza maafa ya wanajeshi na raia pia.Vikosi vya kimataifa vinavyolinda amani nchini Afghanistan-ISAF,chini ya uongozi wa NATO, visiwape wanamgambo wa Kitaliban fursa ya kujipenyeza vijijini na katika miji mikubwa.Hao lazima wazuiliwe njiani.Na hiyo ni sababu ya kuhimiza kuwa ndege za upelelezi za Ujerumani, aina ya Tornado,zikiwa na uwezo wa pekee, zipelekwe haraka nchini Afghanistan.Kwani nguvu ya vikosi vya ISAF ni ubora wa kifundi huko angani,lamalizia WESER-KURIER.