Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 26.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa Magazeti ya Ujerumani

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo hii ni mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya uliofanywa mjini Berlin,kusherehekea miaka 50 tangu kuundwa kwa umoja huo pamoja na kutiwa saini Azimio la Berlin.

Moja kwa moja tutaanza na mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na maoni ya gazeti la SUDDEUTSCHE ZEITUNG ambalo lina mashaka yake,licha ya maafikiano kupatikana kwenye mkutano huo wa kilele,kutafuta suluhisho la mgogoro wa katiba ya Ulaya.Likiendelea linasema:

Haitoshi tu kuafikiana tarehe za kukutana kwani Azimio la Berlin linadhihirisha kuwa njia ya kuelekea kwenye Katiba ya Ulaya ni ndefu mno.Ikiwa mikataba ya asili kuhusika na katiba haitokuwa sehemu ya katiba mpya,basi Ulaya itajikuta katika mzozo usio na mwisho.

Lakini gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linamatumani.Linasema,ni muda mrefu sana tangu Umoja wa Ulaya kupata kujisifu.Mjini Berlin ambako viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya walikusanyika kusherehekea miaka 50 tangu kuundwa kwa umoja huo,maadali ya pamoja yamesifiwa na mktaba wa kihistoria umeimarishwa.Baada ya muda mrefu,umoja huo kwa mara nyingine tena umesisitiza yale yanayofungamanisha na si yanayotenganisha.

Gazeti la ABENDZEITUNG pia limejishughulisha na mada ya Umoja wa Ulaya,lakini linatupia jicho ukosoaji wa Baba Mtakatifu kwamba imani ya kidini haikutajwa katika Azimio la Berlin lililotiwa saini na viongozi wa Umoja wa Ulaya.Gazeti hilo likiendelea linasema,kinachosumbua ni kwamba hapo ni Wakristo na hasa Wakatoliki ndio wangehusika. Lakini Azimio la Berlin limeingiza kila kitu: kuanzia maadili hadi haki za binadamu,yaani kiini ni kuhifadhi heshima ya binadamu,kuwa na usawa, kustahmiliana,kushikamana na kuheshimiana.Hayo ni maadili mema ya Ulaya yenye fahari na ambayo ni sehemu ya Ukristo lakini si Ukristo peke yake. Kwani Umoja wa Ulaya,si tawi dogo la Vatikan laongezea ABENDZEITUNG.

Sasa tunatupia jicho mada nyingine inayohusika na tangazo kuwa Porsche-kampuni inayotengeneza magari ya fahari yenye mwendo mkubwa inaongeza sehemu ya hisa zake katika kampuni ya gari VW kwa kiwango ambacho Porsche itaweza kupendekeza kuinunua VW.Gazeti la HEILBRONNER STIMME linasema katika siku zijazo,kampuni ya Porsche na jimbo la Niedersachsen zitakuwa na wingi mkubwa katika VW.Kwa hivyo,kampuni ya VW haiwezi kununuliwa na wawekezaji na kuvunjwa kuwa matawi mbali mbali.

Sasa maoni ya gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN kutoka mji wa Stuttgart ambako magari ya spoti ya Porsche hutengenezwa.Gazeti hilo,baada ya kuchambua mkakati wa mkuu wa kampuni ya Porsche, Wendelin Wiedeking wa kudhibiti hisa za kutosha ili kuzuia kampuni ya VW kununuliwa na wawekezaji wengine,linasema,sasa ndoto ya Ferdinand Piech anaemiliki sehemu ya kampuni ya Porsche inakaribia kuwa kweli.Piech aliekumbana na mitihani mikubwa ya kashfa,sasa anachukua hatua kubwa ya kudhibiti kampuni ya VW na anasaidiwa pia na Porsche lamalizia Stuttgarater Zeitung.