1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Zimbabwe

20 Aprili 2008
https://p.dw.com/p/Dl2z

Harare:

Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe, imesema kwamba zoezi la kuhesabiwa kura upya katika majimbo 23 kutokana na uchaguzi wa mwezi uliopita, huenda likachukua zaidi ya siku tatu zilizofdikiriwa hapo awali. Naibu mwenyekiti wa tume hiyo ya uchaguzi Utoile Silaigwana alisema sababu ni kwamba hilo si zoezi dogo na wanataka kuhakikisha kuwa hakuna matatizo yanayojitokeza safari hii. Kuhesabiwa kura upya katika majimbo hayo kunafuatia malalamiko ya chama tawala ZANU-PF baada ya kushindwa katika majimbo hayo yote na chama cha upinzani Movement for Democratic Change MDC.Msemaji wa chama hicho Nelson Chamisa amedai kuna mizengwe inayofanyika, akiushutumu utawala wa rais Robert Mugabe kuwa unacheza na wananchi. Akaongeza kwamba ni dhahiri kwamba tume ya uchaguzi ni tawi la chama tawala Zanu-Pf.

Johannesburg:

Viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika wameshutumiwa vikali kwa msimamo wao laini kuhusu matukio nchini Zimbabwe. Wakati Rais wa Marekani George W. Bush na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon wamewataka viongozi wa jumuiya ya amaendeleo kusini mwa Afrika-SADC kuchukua msimamo wa ujasiri zaidi , jumuiya hiyo inaelekea bado kutegemea upataanishi wa rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini ambaye anakataa kuwa kuna mgogoro Zimbabwe. Ombi la upinzani kutaka Mbeki ajiondoe na nafasi yake ichukuliwe na rais Levy Mwanawasa wa Zambia hadi sasa halielekei kupewa uzito na nyingi miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Zambia ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya SADC.