Uchaguzi waanza Jamhuri ya Afrika ya Kati | Matukio ya Afrika | DW | 30.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Uchaguzi waanza Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wanajeshi wa kulinda amani wanapiga doria katika mitaa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, wakati raia wakishiriki uchaguzi wa rais na bunge unaonuiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia baada ya miaka kadhaa ya mzozo wa kidini.

Zentralafrikanische Republik Referendum

Misururu mirefu ya watu nje ya vituo vya kupigia kura mjini Bangui

Misururu mirefu ya watu imeonekana katika vituo vya kupigia kura mjini Bangui na katika eneo la Waislamu la PK5, huku wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria katika maeneo hayo na kuyaegesha magari yao karibu na vituo vya kupigia kura.

Takriban wagombea 30 wanapigania kiti cha Uraisi, lakini kufuatia kukosekana kwa uchunguzi wa maoni au rais anayewania nafasi yake, imekuwa vigumu kutabiri mshindi wa uchaguzi huo. Hata hivyo wagombea wanaoonekana kuwa na nafasi nzuri ya kuongoza ni Waziri Mkuu wa zamani Anicet-Georges Dologuele na Martin Ziguele.

Ziguele alipata uungaji mkono hapo jana kutoka kwa waasi wa anti balaka waliyounda chama cha muungano na maendeleo cha Jamhuri ya Afrika ya Kati, waliposema wanaunga mkono hatua yake ya kugombea.

Zentralafrikanische Republik Wahlen Demonstration

Wanajeshi wa Kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Wagombea wengine ni pamoja na Waziri wa zamani wa mambo ya nje Karim Meckassoua, na Bilal Desire Nzanga-Kolingba, mtoto wa rais wa zamani.

"Tumekuja kupiga kura kwa sababu tunataka kuwa huru na turejee katika taaluma zetu, tunataka kukomesha mapigano," alisema mfanya biashara mmoja mjini Bangui Gradias Vara.

"Tutamchagua rais ambaye ni mzuri kwa nchi hii," alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja tu Lucie. Kwa upande mwengine Faustin Archange Touadera, mgombea wa kujisimamia amesema uchaguzi utaiwezesha nchi kuwa na rais halali, kigezo muhimu cha kumaliza mzozo Jamhuri ya Afrika ya kati.

Raia wasema wanamatumaini ya kuwepo mabadiliko baada ya uchaguzi.

Kando na uchaguzi kuanza kuchelewa kufuatia matayarisho kuchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, watu wengi mjini Bangui wamesema wanatumai uchaguzi huu utaleta mabadiliko katika nchi hiyo iliyoongozwa tangu Mei mwaka wa 2014 na rais wa mpito Catherine Samba-Panza, ambaye sheria inambana kugombea.

Kwa upande mwengine kundi la waasi wa Seleka lilijiondoa mjini Bangui baada ya kiongozi wake Michel Djotodia kujiondoa kama raisi mwaka wa 2014 na kujikusanya katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Catherine Samba-Panza 2014 Präsident Zentralafrikanische Republik

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza

Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa saa kumi na moja jioni huku matokeo ya mwanzo yakitarajiwa kuanza kutolewa siku zinazofuata. Mahakama ya katiba hata hivyo inapaswa kutoa rasmi matokeo ya mwisho ya uchaguzi siku 15 baada ya zoezi la uchaguzi kufanyika. Wagombea wengine wengi pia wanashiriki katika uchaguzi wa bunge.

Msukosuko wa kisiasa na vurugu mjini Bangui mwezi wa Septemba iliilazimisha serikali kuahirisha uchaguzi huku wengine wakiwa na mashaka iwapo uchaguzi huo utaandaliwa kwa mafanikio.

Hapo jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitoa wito wa kuwepo uchaguzi wa amani na wa kuaminika. Ban amesema hatua ya watu milioni 2 kujiandikisha kupiga kura, inaonesha wazi nia ya raia ya kutaka kuirejesha nchi katika utawala wa kidemokrasia.

Mwandishi: Amina Abubakar/REUTERS/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga