Uchaguzi wa Rais Malawi. | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.05.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Rais Malawi.

Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi amezidi kujihakikishia ushindi leo kwa kuongoza kwa kura nyingi kufuatia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika siku ya Jumanne.

Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika.

Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo, Rais Bingu wa Mutharika anaongoza kwa wingi mkubwa.


Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo Anastasia Msosa amesema tayari kura zimehesabiwa na kuthibitishwa kutoka katika majimbo 153 kati ya majimbo 193 ya uchaguzi ikiwa ni karibu asilimia 80 na kwamba matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa muda wowote kutoka sasa.


Hata hivyo Kiongozi wa upinzani nchini humo John Tembo amesema leo kwamba uchaguzi huo uliofanyika nchini humo ulikuwa na udanganyifu na atakwenda Mahakamani kupinga matokeo.


Akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa Habari amesema amepokea malalamiko kutoka sehemu mbalimbali nchini humo na anaamini kuwa wanaushahidi wa kutosha kuonesha kuwa uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu.


Lakini kwa upande wake Rais wa zamani wa nchi hiyo ambaye pia ni kiongozi wa chama cha upinzani cha United Democratic Front Bakili Muluzi ambaye alizuiliwa na mahakama kushiriki katika uchaguzi huo kuwania nafasi ya Urais na badala yake kumuunga mkono John Tembo katika uchaguzi huo, amekiri kuwa Rais Mutharika ameshinda uchaguzi huo na kuahidi kuunga mkono serikali mpya.


Kwa upande wao, Waangalizi wa Kimataifa katika Uchaguzi huo wamemlaumu Rais Bingu wa Mutharika kwa kutumia vyombo vya habari vya taifa na rasilimali nyingine za nchi, kumpendelea yeye katika uchaguzi huo.


Kwa upande wake Kiongozi wa wa kundi la Waangalizi kutoka Jumuia ya Madola Rais wa zamani wa Ghana John Kufuor, ripoti na taarifa nyingi za matukio ya Rais na chama cha Democratic Progressive DPP zilikuwa zikifanyiwa kampeni na Radio ya Taifa jambo ambalo amelielezea kuwa ni ushabiki wa kisiasa usio na aibu.


Kiongozi wa timu ya Waangalizi wa Umoja wa Ulaya Luisa Morgantini ameelezea utumiwaji mbaya wa mali za serikali wakati wa kampeni za uchaguzi huo, ambavyo ametolea mfano vyombo vya habari, pamoja na utumiaji wa magari ya serikali, polisi na pamoja na huduma nyingine za ulinzi.


Wakizungumza kuhusiana na ripoti yao ya awali kuhusiana na uchaguzi mkuu nchini Malawi, Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamesema Uchaguzi wa nne wa Vyama vingi uliofanyika nchini humo wiki hii umekuwa na kasoro nyingi ambazo zinaonesha wazi umuhimu wa kuendelea na mabadiliko nchini humo.


Wamesema wakati wa kipindi cha kampeni idadi ya matatizo ilionesha wazi udhaifu uliopo, ambao unahitaji kuelezwa ili Malawi iweze kutimiza viwango vya kimataifa na kikanda katika chaguzi zake.


Ripoti kamili ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na uchaguzi huo inaweza kutolewa katika kipindi cha miezi miwili

Uchaguzi huo mkuu nchini Malawi pia uliharibiwa kwa kukamatwa kwa Waandishi wa Habari waliokuwa wakifanya kazi katika Radio iliyokuwa ikiunga mkono Upinzani.


Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri:M.Abdul-Rahman
 • Tarehe 21.05.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/Reuters
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HupJ
 • Tarehe 21.05.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza/Reuters
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HupJ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com