Uchaguzi wa Rais Brazil kuelekea duru ya pili | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Rais Brazil kuelekea duru ya pili

Rais wa Brazil Dilma Rousseff anakabiliwa na kinyanganyiro kigumu baada ya kushindwa kupata kura zinazohitajika kumuepusha kuingia katika duru ya pili. Rousseff atakutana na Aecio Neves katika duru ya pili Oktoba 26

Neves ambaye ni gavana wa zamani na seneta,amekuwa hachukuliki kama mgombea mwenye kutoa kitisho chochote cha kutia wasiwasi kwa kambi ya Rouseff hadi siku chache za kampeini kabla ya uchaguzi uliofanyika hapo jana.

Huku karibu kura zote zikiwa zimehesabiwa,Rousseff amepata asilimia 41 na Neves amepata asilimia 34 huku waziri wa mazingira aliyekuwa na umaarufu mkubwa Marina Silva ambaye alikuwa akipigiwa upatu kushinda ambaye angekuwa Rais wa kwanza mweusi akiwa katika nafasi ya tatu kwa asilimia 21.

Rousseff anapigiwa upatu kushinda

Bi Rousseff anaonekana kuwa atashinda awamu ya pili ya kipindi cha uongozi cha miaka minne ijayo na kuendeleza uongozi wa chama tawala cha wafanyakazi PT, ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 12, wakati duru ya pili ikitarajiwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu.

Rais wa Brazil Dilma Rousseff

Rais wa Brazil Dilma Rousseff

Kampeini za duru ya pili ya uchaguzi huo zitajikita kati ya ahadi za chama tawala kuhusu maendeleo huku kiking'angana kuufufua uchumi wa Brazil ambao uliporomoka mwanzoni mwa mwaka huu dhidi ya sera za chama cha Neves cha Social Democracy PSDB ambacho kinaahidi sera zinazotoa mazingira bora kwa soko la kibiashara la Brazil.

Akisherehekea ushindi wa duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi,Rouseff amesema Brazil haiwezi kurudi nyuma na kusema ameelewa ujumbe uliotoka kutoka barabarani na katika masanduku ya kupigia kura kuwa wengi wa raia wake wanataka waharakishe kuijenga nchi hiyo.

Kwa upande wake, Neves anayeungwa mkono na matajiri ameahidi kuendelea kubeba mwenge wa mabadiliko na kuwarai wafuasi wa mpinzani wake Silva wa chama cha kisosholisti kuwa ni wakati sasa wa kuungana kuyaleta mageuzi hayo.

Hata hivyo Silva ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha PT hakukimbilia kutangaza kuwa atamuunga yeyote kati ya wagombea hao katika duru ya pili.

Neves atoa ushindani usiotarajiwa

Rousseff mwenye umri wa miaka 66 yuko katika nafasi ngumu kutokana na uchumi wa Brazil kuendelea kushuka kwa mwaka wa nne mfululizo na kuimarika ghafla kwa Neves kwenye kinyang'anyiro hicho ambaye kura za maoni za kabla ya uchaguzi wa jana zilikuwa zimemuweka katika nafasi ya tatu.

Mgombea wa urais Brazil Aecio Neves

Mgombea wa urais Brazil Aecio Neves

Wachambuzi wanasema ili Neves mwenye umri wa miaka 54 ashinde,anahitaji kuwashawishi wapiga kura kuwa ahadi zake za kuufufua uchumi hazitaathiri mipango iliyopo ya kuisaidia jamii hasa ule wa kutolewa fedha ambazo familia za tabaka la chini hupewa kila mwezi na serikali ili kuhakikisha watoto wao wanasalia shuleni. Neves ameahidi kuudumisha mpango huo.

Hata hivyo bado wapiga kura wengi wanasema wako tayari kumpa Rousseff na chama chake nafasi nyingine ya kusawazisha matatizo yaliyopo nchini humo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com