1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mji wa Istanbul Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Juni 2019

Ushindi wa upande wa upinzani katika uchaguzi wa baraza la mji wa Istanbul, na vitisho vya makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya wanasiasa ni miongoni ma mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3Kyus
Istanbul-Wahl Ekrem Imamoglu  (Onur Günal)
Picha: picture-alliance/dpa/O.Gunay

 

Tunaanzia Uturuki ambako matokeo ya uchaguzi uliorudiwa wa baraza la mji wa Istanbul yamethibitisha ushindi wa upande wa upinzani. Hakuna gazeti la Ujerumani ambalo halikuchambua matokeo hayo. "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Matokeo ya uchaguzi sio tu ni ushindi kwa Imamoglu, bali pia  ni onyo kwa kiongozi wa nchi hiyo: Erdogan hawezi tena kujinata hawezi kushindwa. Alianza kujipatia umashuhuri mwaka 1994 alipokuwa meya wa Istanbul. Miaka 25 baadae, matokeo hayo ya uchaguzi yanaweza kuashiria mwanzo wa kuporomoka kwake kisiasa. Lakini zaidi kuliko yote, matokeo ya uchaguzi wa jiji la Istanbul ni ushindi kwa mfumo wa demokrasia nchini Uturuki."

 Gazeti la Badische Zeitung linajiuliza  rais Erdogan na chama chake cha AKP watasema nini tena baada ya matokeo hayo kutangazwa? Gazeti linaendelea kuandika:"Eti watashuku kwa mara nyengine tena? Au Erdogan atatekeleza vitisho alivyotoa vya kumfikisha mahakamani mshindi na kumuapisha badala yake mtu anaemtaka! Uamuzi kama huo sio tu utazusha hasira miongoni mwa wananchi bali pia utaitumbukiza Uturuki katika zahma ya machafuko yasiyokuwa na mfano. Uchaguzi umeshapita, Erdogan anabidi akubali anaweza pia kushindwa."

Vitisho vya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia

Mjadala umepamba moto kufuatia kisa cha kuuliwa meya wa mji wa Kassel katika jimbo la Hesse Wolter Lübcke na mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Chanzo cha mauwaji ni msimamo wake kuelekea wahamiaji. Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu Horst Seehofer anataka wanyimwe haki msingi wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Gazeti la "Badische Meueste Nachrichten" linaandika: "Hiyo sio njia ya maana anayoichonga waziri. Na pengine inaweza kuwa ya hatari. Kwasababu taifa linalofuata sheria limejengeka kwa msingi wa kudhamini haki msingi kwa kila raia, mwanamke kwa mwanamme, kila mgeni, kila mwenye kuomba kinga ya ukimbizi, kila mhalifu na kila mnazi mambo leo. Hilo linaumiza baadhi ya wakati, lakini ni la lazima na hivyo ndivyo taifa linalofuata sheria linavyofanyakazi."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Sekione Kitojo