1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Afrika Kusini mtihani kwa Ramaphosa

Grace Kabogo
8 Mei 2019

Wananchi wa Afrika Kusini leo wamepiga kura kuwachagua rais na wabunge katika uchaguzi mkuu wa sita wa kidemokrasia tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1994.

https://p.dw.com/p/3IBPc
Südafrika Wahlen Wähler in Johannesburg
Picha: Reuters/M. Hutchings

Chama cha African National Congress, ANC cha Nelson Mandela ambacho kimekuwepo madarakani tangu mwaka 1994 kinapewa uwezo mkubwa wa kushinda katika uchaguzi huo, ingawa kinakabiliwa na changamoto ya kuzishikilia asilimia 62 ya kura ambazo ilizipata katika uchaguzi wa miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo, dalili za awali zinaonesha kuwa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni ndogo, kutokana na wapiga kura kuvunjika moyo kwa sababu ya kashfa za rushwa na ukosefu wa ajira.

Akizungumza baada ya kupiga kura yake katika shule ya Chiawelo, Soweto, Rais Cyril Ramaphosa amesema ana uhakika mkubwa wa matokeo mazuri na amefurahishwa na idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura.

Südafrika - Wahl / Präsident Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa (katikati) akiwa na wafuasi wa chama cha ANC Picha: picture-alliance/B. Curtis

''Huu ni uchaguzi ambao unatukumbusha mwaka 1994, kwa sababu mwaka huo watu wetu walikuwa na msisimko kama huu,  walikuwa wanaingia kwenye ukurasa mpya, mustakabali mpya wa nchi yetu.

Na leo wanataka kuichagua serikali ambayo itawahudumia, ambayo itayashughulikia madai yao, matarajio yao na wana uhakika mkubwa kwamba tunaweza kufanya hivyo,'' alisisitiza Ramaphosa.

Awali katika kampeni, Ramaphosa aliahidi kukisafisha chama chake cha ANC ambacho kinakabiliwa ma madai ya rushwa na matatizo ya kiuchumi, huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa kimeongezeka kwa kiasi ya asilimia 27, matatizo ambayo yalimlazimisha mtangulizi wake Jacob Zuma kujiuzulu mwaka uliopita.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Economic Freedom Fighters, EFF, Julius Malema amesema anatarajia matokeo mazuri kwa chama chake. Hayo ameyazungumza baada ya kupiga kura kwenye mji wa Seshego, kaskazini mwa jimbo la Limpopo.

Julius Malema
Kiongozi wa EFF, Julius MalemaPicha: dapd/AP Photo/Themba Hadebe

''Kama watu wanataka kuendelea kukosa ajira, kama watu wanataka kuendelea kuishi bila ardhi, wanaweza kuendelea kukipigia kura chama cha ANC,'' alisema Malema.

Wananchi wa Afrika Kusini wanawachagua wabunge na viongozi wa majimbo tisa ya nchi hiyo. Waafrika Kusini milioni 26.7, ambayo ni karibu nusu ya watu wote wa nchi hiyo walijiandikisha kupiga kura, katika vituo 22,925 vilivyofunguliwa tangu mapema leo asubuhi.

Vyama 48 vinashiriki katika uchaguzi huo mkuu. Matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa kesho Alhamisi na matokeo rasmi yanapaswa kutangazwa ndani ya siku saba. Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini inatarajiwa kumtangaza rasmi mshindi siku ya Jumamosi. Kikao cha kwanza cha bunge la Afrika Kusini kimepangwa kufanyika Mei 22.