Uchaguzi wa Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Afghanistan

Vikosi vya taifa na vya kimataifa vajiandaa kuhakikisha usalama,uchaguzi utakapoitishwa Afghanistan

default

Rais Hamid Karsai atetea wadhifa wake

Licha ya mashambulio ya kigaidi katika mtaa wa mabalozi mjini Kabul,uchaguzi wa rais utafanyika kama ilivyopangwa nchini Afghanistan.Vikosi vya usalama tangu vya ndani mpaka vya kimataifa vimepania kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha uchaguzi unapita kama inavyotakikana.

Maandalizi ya uchaguzi si kazi rahisi.Wananchi milioni 17 wameandikishwa kupiga kura.Kamisheni huru ya uchaguzi inabidi kupeleka vyeti vya upigaji kura,wino kwaajili ya kuchora vyeti vya kupiga kura na kupaka vidole vya wapiga kura pamoja na vifaa vyenginevyo,katika vituo 29 000 kote nchini Afghanistan.

Kutokana na kitisho cha kutokea mashambulio ya kigaidi,vikosi vya jeshi la taifa na vile vya kimataifa vya ISAF vimepanga kushirikiana kwa dhati kusimamia usalama wakati wa uchaguzi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Zmarai Bashari anasema:

"Mkakati wa usalama tuliouandaa unazungumzia juu ya kuwepo maeneo manne ya usalama:Katika eneo la kwanza ambalo ni karibu na vituo vya kupiga kura,watawekwa askari polisi wa taifa.Katika eneo la pili watawekwa wanajeshi wa taifa.Katika eneo la tatu watawekwa wanajeshi wa kimataifa na eneo la nne wanaanga wa jeshi la kimataifa,watapiga doria."

Msemaji wa wizara ya ulinzi Zaher Azimi anasisitiza juu ya umuhimu wa kuwajibika raia wa kawaida katika kuhakikisha usalama.

Kinyume na hali namna ilivyokua uchaguzi wa rais ulipoitishwa miaka mitano iliyopita,safari hii vikosi vya jeshi la Afghanistan vinakamata mstari wa mbele katika kuandaa,kusimamia na kudhamini utaratibu mzima wa uchaguzi.Wanajeshi laki mbili na nusu watasimamia utaratibu wa kupiga kura kote nchini Afghanistan.Watasaidia na wasimamizi laki moja na nusu wa kiraia.

Lakini kuna maeneo ambayo vikosi vya usalama vya Afghanistan na vile vya kimataifa havitatia mguu.Mfano katika maeneo ya kusini ambako wanamgambo wa Taliban wanatishia kuufuja uchaguzi huo.

ISAF Soldaten der Bundeswehr Afghanistan

Wanajeshi wa Ujerumani walinda amani nchini Afghanistan

Katika maeneo ya kaskazini,walikowekwa wanajeshi wa kikosi cha kimataifa cha ISAF kinachowajumuisha wanajeshi wa Ujerumani,hali ni afadhali.Akihojiwa na DW luteni kanali Michael Weckbach,alisema:

"Tuna wanajeshi 5800 kutoka mataifa 14.Watajitahidi kuhakikisha auchaguzi unapita salama, kwa ushirikiano pamoja na vikosi vya Afghanistan.Ingawa tunaamini hata huku fujo za hapa na palke zinaweza kutokea,lakini hazitakua fujo za kuweza kukorofisha uchaguzi.

Mamia ya wasimamizi tangu wa kutoka ndani mpaka nje ya Afghanistan watashuhudia uchaguzi huo ambao walimwengu wanataraji utakua wa haki na utapita katika hali ya uwazi.

Mwandishi:Dr. Samimy Musa / Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Othman Miraji

 • Tarehe 17.08.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JCxM
 • Tarehe 17.08.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JCxM
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com