1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Sudan

19 Oktoba 2010

Jeshi la Sudan limepinga mpango wa umoja wa mataifa kutaka kuweka wanajeshi wa kulinda amani kwenye mipaka

https://p.dw.com/p/Pg0a

KHARTOUM

Jeshi la Sudan limepinga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kuweka wanajeshi wa kulinda amani kwenye mpaka kati ya kaskazini na kusini mwa Sudan kabla ya wakaazi wa eneo hilo la kusini kupiga kura ya maoni mwakani. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Tribune.

Msemaji wa jeshi hilo Al-Sawarmi Khalid Sa'ad amenukuliwa akisema serikali ya Sudan ina uwezo wa kuhakikisha hali ya usalama. Aliongezea kuwa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan-UNMIS havina mamlaka ya kupeleka wanajeshi wake kwenye mpaka wa eneo la kaskazini na lile la kusini ambalo kwa sehemu fulani linajitawala lenyewe.

Hapo awali, mkuu wa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, Alain Le Roy alitangaza mpango wa kupeleka wanajeshi hao. Amesema lengo ni kuzuia matukio ya ghasia wakati wa kupigwa kura ya maoni Januari 9 mwakani. Kura hiyo itaamua iwapo eneo la Sudan Kusini litakuwa huru au litabakia sehemu ya taifa la Sudan.

Mwandishi: Sekione Kitojo/zr

Mhariri: Aboubakar Liongo