1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu wanukia Uingereza?

Saumu Mwasimba
23 Septemba 2018

Chama kikuu cha upinzani cha Labour chasema serikali ya waziri mkuu May iko ukingoni kuelekea kuporomoka na kuna uwezekano wa kuwepo haja ya uchaguzi mkuu kuitishwa ikiwa mpango wake wa Brexit utashindwa

https://p.dw.com/p/35MAm
Uk | Wahlkampf Theresa May 2017
Picha: Getty Images/J. Tallis

Naibu kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza cha Labour, Tom Watson amesema serikali ya waziri mkuu Theresa May iko ukingoni kuelekea kuporomoka na kuna uwezekano wa kufanyika uchaguzi mkuu hivi karibuni. Katika mkutano mkuu wa kila mwaka wa chama cha Labour unaofanyika katika mji wa Liverpool, Watson amebaini kwamba ikiwa wananchi wa Uingereza wataunga mkono fikra ya kufanyika duru kwa mara ya pili kura ya maoni kuhusu Brexit basi itakuwa vigumu kwa uongozi wa chama hicho kupuuza hilo.

Kadhalika waziri kivuli wa masuala ya biashara na nishati wa chama hicho cha Labour Rebecca Long Bailey amesisitiza kwamba panahitajika uchaguzi wa kitaifa ikiwa Thresa May atashindwa kupata uungwaji mkono bungeni katika mpango wake wa Brexit. Ingawa pia amesema uongozi wa Labour haujaunga mkono fikra ya kufanyika kwa mara ya pili kura ya maoni kuhusu mpango wa mwisho wa Uingereza kujiondowa katika Umoja wa Ulaya.

Europa UK l Symbolbild Brexit
Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Lakini pia Bailey amesema chama cha Labour kitaheshimu uamuzi wowote wa wanachama wake katika mkutano huo wa Liverpool katika kuunga mkono fikra hiyo. Baileys pia amekiambia kituo cha habari cha SKyNews kwamba msimamo wa Labour ni kutaka kuitishwe uchaguzi mkuu ikiwa Theresa May hatoweza kuungwa mkono bungeni au hata na chama chake kuendelea na mpango wake. Pamoja na hayo mapendekezo ya waziri mkuu May ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya-Brexit yanaonekana hayana uhai na serikali pamoja na viongozi wa Umoja wa Ulaya wanahitaji kutazama kwa kiasi gani mazungumzo yanaweza kuendelea. Hilo ni wazo ambalo limetolewa na mbunge anayeunga mkono Umoja wa Ulaya kutoka chama cha bibi Theresa May cha Conservative.

Großbritannien Jeremy Corbyn in London
Picha: picture-alliance/ZUMA/London News Pictures/T. Akmen

Katika mkutano wa kilele uliofanyika nchini Austria wiki iliyopita viongozi wa Umoja wa Ulaya walioukataa katakata mpango wa May wakisema waziri mkuu huyo anahitajika kutowa maelezo ya msingi kuhusu suala la biashara na mipango ya forodha inapohusika mipaka ya Uingereza na Ireland.

Na hatua hiyo ndiyo inayoelezwa na Nicky Morgan ambaye ni mwenyekiti wa kamati maalum ya bunge kuhusu hazina ambaye pia aliwahi kuwa waziri kwamba inafanya kutokuwepo uhakika ikiwa mpango wa waziri mkuu una uhai.

Kwa hivi sasa kinachojitokeza kutoka Uingereza kwa mujibu wa yale yanayozungumzwa na viongozi wa chama cha Labour wakati huu huko Liverpool ni kwamba serikali ya Thresa May inapingwa kwa kiasi kikubwa katika mpango wake wa Brexit na hata wanachama wa chama cha Conservative wenyewe.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/afp/reuters

Mhariri