1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji yageuka maficho ya magaidi

Daniel Henrich/Saumu Mwasimba18 Novemba 2015

Katika miaka kadhaa iliyopita nchi hiyo imejikuta ikigeuka kuwa kiini cha kuongezeka kwa makundi ya itikadi kali. Wengi wa watuhumiwa wanatokea katika jamii za wenye hali ngumu za kiuchumi.

https://p.dw.com/p/1H7iG
Polisi katika mtaa wa Molenbeek, Ubelgiji
Picha: Reuters/Y. Herman

Kwa mtaalamu wa masuala ya kisiasa Asiem El Difraoui matatizo ya ugaidi nchini Ubelgiji ni ya kujitakia.Mtaalamu huyo anasema wabelgiji wamekuwa wakitazama hali na kuiachia ishamiri,walishindwa kuchukua hatua za kuzuia kushamiri huko na kwa hivyo kwa jicho la mtaalamu huyo wa siasa za mashariki ya kati akizungumza na DW anasema kwa hakika yote wameyakuza wenyewe. Aidha kushindwa kwa vita dhidi ya ugaidi anavyoona mtaalamu huyo kunatokana na sababu kuu moja ya wazi nayo ni mzozo wa ndani unaoizunguka nchi hiyo.

Anasema tatizo lilipo hasa ni kwamba wabelgiji wamekuwa wakijikita tu katika kushughulikia masuala yanayowahusu wenyewe tu. Kwa miaka mingi wamekuwa wenyewe kwa wenyewe wakifarakana baina ya waflemish na waloni kwa hali ambayo imekuwa ikisababisha matatizo hata katika kushughulikia siasa za ndani za taifa hilo.

Wapiganaji kutok Ubelgiji waungana na IS Iraq na Syria

Kwa mujibu wa kituo kinachojihusisha kufuatilia masuala ya siasa kali na migogoro ya kisiasa kilichoko London Uingereza ICSR kuna haja ya hatua za haraka kuchukuliwa. Shirika hilo linasema utafiti umebaini kati ya mwishoni mwa mwaka 2011 na mwishoni mwa mwaka 2013 hadi wapiganaji 11,000 wamekwenda kupigana sambamba na makundi ya itikadi kali nchini Syria na Iraq, na miongoni mwa wapiganaji hao takriban mmoja kati ya watano anatokea katika nchi za Ulaya ya magharibi.

Vikosi maalumu vikisaka magaidi mjini Verviers, Ubelgiji
Vikosi maalumu vikisaka magaidi mjini Verviers, UbelgijiPicha: Reuters/Stringer

Wapiganaji kiasi 296 wanasemekana kutokea Ubelgiji idadi ambayo inaonesha wazi kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa wanakotokea wapiganaji wengi wa Itikadi kali kutoka nchi za Ulaya. Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa kwa mfano na wale wanaotokea nchi kama Ujerumani ambayo inasemekana kiasi 240 wamejiunga na vita hivyo wanavyoviita vitakatifu.

Waislamu hawajajumuishwa vyema katika jamii

Kwa maneno mengine, inaonesha kwamba katika kila wakaazi milioni moja wa Ubelgiji 27 ni wapiganaji wa itikadi kali hivyo basi ni kusema Ubelgiji ndiyo nchi inayotokea kiwango kikubwa cha wenye itikali kali barani Ulaya. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na na chuo kikuu cha Liege mji mdogo wa Vervier ulioko Mashariki mwa Ubelgiji umegeuka kuwa mfano wa kivutio cha wanaofuata uislamu wa itikadi kali miongoni mwa raia wa nchi hiyo.

Waliofanya utafiti huo wameangalia hali ya maisha katika mji huo halikadhalika suala zima la kuzijumuisha katika mfumo, jamii za watu wanaoishi kwenye mji huo ambao ni mji mojawapo masikini kabisa nchini Ubelgiji. Kati ya wakaazi 53,000 wa mji huo kiasi asimilia 15 ni wageni.

Kiasi asilimia 6 ya Wabelgiji ni waislamu lakini pamoja na kuzungumza lugha kwa ufasaha au hata wabelgiji asili walio waislamu wanaangaliwa kama wageni na hivyo basi kujikuta mara zote wakibaguliwa pale wanapotafuta ajira. Matatizo kama hayo yametajwa kuwa chachu ya kusababisha ghadhabu na kutoa mwanya kwa makundi ya itikadi kali kuwashawishi watu kirahisi kujiunga na itikadi kali.

Mwandishi: Daniel Henrich/Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman