1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uasi wa Ghetto la Warsaw, miaka 80 baadae

Iddi Ssessanga
19 Aprili 2023

Miaka 80 iliyopita, Wayahudi waliofungwa katika Ghetto la Warsaw nchini Poland waliasi dhidi ya wakaliaji wa Ujerumani. Kilikuwa kitendo kikubwa zaidi cha upinzani wa Wayahudi dhidi ya Wanazi.

https://p.dw.com/p/4QHyX
Warschauer Aufstand Nazi Verbrecher
Picha: AP

Marais na watu walionusurika na mauaji ya Holocaust pamoja na vizazi vyao hii leo wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya kile kinachofahamika kama uasi wa Ghetto, katika hatua inayoashiria kwamba jukumu la kubeba kumbukumbu ya mauaji hayo linahama kutoka kwa walioshuhudia kwenda kwa vizazi vyao.

Kumbukumbu hiyo inawaenzi mamia ya vijana wa Kiyahudi waliobeba silaha mjini Warsaw mwaka 1943 dhidi ya jeshi lenye nguvu la manazi wa Ujerumani, na hiki ndiyo kilikuwa kitendo kikubwa zaidi cha upinzani wao dhidi ya utawala wa wanazi.

Wajerumani ambao waliikalia Poland tangu msimu wa mapukutiko wa mwaka 1939, waliunda Ghetto hilo mnamo Oktoba 1940, likiwa Ghetto kubwa zaidi la Wayahudi katika maeneo yaliokaliwa ya Ulaya, na ni kutokea hapo ambapo watu 300,000 walipelekwa kuuawa katika vyumba vya gesi vilivyokuwa katika kambi mbalimbali za mauaji.

 Marek Edelman Kommandeur Aufstand im Warschauer Ghetto von 1943
Kamanda wa mwisho wa upinzani wa Wayahudi dhidi ya manazi, Marek Edelman, alifariki dunia mwaka 2009.Picha: Pawel Supernak/dpa/picture-alliance

Hakuna manusura wapiganaji walio hai hivi sasa, ambapo kamanda wa mwisho Marek Edelman alifariki dunia mwaka 2009. Alisalia nchini Poland na kuaidia kuweka hai kumbukumbu ya uasi huo katika taifa lake la nyumbani.

Soma pia: Poland na miaka 75 ya uasi wa Wayahudi dhidi ya Wanazi

Simcha Rotem, mpiganaji aliewatorosha wengine kutoka ghetto lililokuwa linawaka moto kupitia mifereje ya uchafu, alifariki mwaka 2019 nchini Israel ambako alihamia, na idadi ndogo ya mashuhuda waliosalia hii leo walikuwa watoto wakati wa uasi huo.

Marais Herzog, Steinmeier, Duda wahudhuria

Kumbukumbu rasmi zitahudhuriwa na marais Isaac Herzog wa Israel, Frank Walter Steinmeier wa Ujerumani, na Andrzej Duda wa Poland, ambapo tukio kuu litafanyika mbele ya mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa ghetto katika mahali ambapo mapigano yalizuka, na baadae watazuru Sinagogi la Nozyk mjini Warsaw, kabla ya tamasha la jioni litakalotumbuizwa na bendi ya Orchestra ya vijana wa Polanda na Israel.

Uasi huo ulianza Aprili 19, 1943 kwa shambulio la risasi dhidi ya safu ya wanajeshi wa Kinazi na wapiganaji wa upinzani wa Kiyahudi, wengi wao wakiwa vijana wa kiume na kike, katika mkesha wa mapumziko ya Pasaka ya Wayahudi.

Siku tatu baadae Wanazi walilichoma moto ghetto hilo, na kuligeuza kuwa tanuru la kifo, lakini wapiganaji wa Kiyahudu waliendelea na mapambano yao kwa karibu mwezi mmoja, kabla ya kusambaratishwa kikatili. Mapambano hayo yalichukuwa muda mrefu zaidi kuliko baadhi ya mataifa yalivyofikiria.

Deportation von jüdischen Frauen und Kindern
Uhamishaji wa wanawake na watoto wa Kiyahudi kutoka Ghetto la Warsaw kupitia mabehewa ya treni kuelekea Treblinka mjini Warsaw.Picha: picture-alliance / IMAGNO/Austrian Archives

Baadhi ya wanaoshiriki katika maadhimisho ya Jumatano walisafiri kutoka mataifa ya mbali kama Australia na Marekani kuwaenzi wale walioangamia, lakini pia ustaarabu tajiri wa Kiyahudi ambao ni urithi wao.

Wengi hufanya sherehe zao za binafsi, kutoa heshima kwa wale waliofariki kwenye makaburi ya Kiyahudi au kwenye kumbukumbu mbalimbali kwenye viwanja vya zamani vya ghetto.

Chanzo: AP,DW