1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uandikishaji wapigakura waingia dosari Kenya

7 Desemba 2012

Huku ikiwa imesalia chini ya wiki moja na nusu kabla ya kufungwa rasmi kwa shughuli ya kuwaandikisha wapiga kura nchini Kenya, shughuli hiyo imekumbwa na dosari ya idadi ndogo ya watu kujitokeza kuandikishwa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/16xT6
Viongozi wa Kenya.
Viongozi wa Kenya.Picha: AP

Katika eneo la Mkoa wa Pwani ambalo limeshuhudia visa vya ukosefu wa amani na kadhalika kutokana na kauli mbiu ya vuguvugu la Mombasa Republican linalopigania ukombozi wa jimbo hilo kwamba Pwani isusie uchaguzi mkuu ujao, wakaazi wengi bado wanahofu ya kujiandikisha kama wapiga kura.

Shughuli hii ambayo ni ya kwanza nchini Kenya kuendeshwa kwa kutumia mitambo ya Komputa inajikokota huku kukiwa na hofu kwamba huenda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka isitimize ndoto yake ya kuwasajili wapiga kura milioni 18 wakati muda huo utakapokamilika tarehe 18 mwezi huu.

Ingawa Mkoa wa Pwani nchini Kenya ni miongoni mwa mikoa iliyoandikisha rekodi bora ya wapiga kura, kufikia sasa ukiwa na jumla ya asilimia mia 24 ya wapiga kura waliojitokeza miongoni mwa wanaotarajiwa kujisajili kutoka eneo hili, bado kuna hali ya wasi wasi miongoni mwa wakaazi wake, kufuatia vitisho vinavyodaiwa kutolewa na wafuasi wa vuguvugu la Mombasa Republican ambalo linadai ukombozi wa jimbo la Pwani.

Ukosefu wa usalama ndio changamoto kubwa, hasa katika maeneo yaliyoshuhudia mauaji ya kikabila mfano Tana River, na eneo la Baragoi ambako askari polisi 48 waliuawa hivi majuzi.

Matokeo ya mashambulizi kwenye Mkoa wa Pwani ya Kenya.
Matokeo ya mashambulizi kwenye Mkoa wa Pwani ya Kenya.Picha: dapd

Aidha eneo la Tana River, ambako zaidi ya watu 100 waliuawa wakati wa mapigano ya kikabila mwezi wa nane,wakaazi wengi bado wana hofu ya kurejea makwao baada ya nyumba zao kuchomwa moto na pamoja na mali zao, huku wakiwa hawana vitambulisho ambavyo ni ngao na stakabadhi muhimu ya Mtu kujiandikisha kama mpigaji kura.

Idara ya utawala mkoani pwani kupitia Kamishna mkuu wa Jimbo la Mombasa Nelson Marwa unatoa onyo kali dhidi ya vitisho hivyo.

Changamoto nyingine ambazo zinajitokeza katika shughuli hii ni kuhusu mitambo ya kisasa ya kuwasajili wapiga kura.

Hii itakuwa mara ya kwanza Kenya kuendesha uchaguzi kwa njia ye electroniki, lakini tayari mitambo hiyo inakumbwa na matatizo katika baadhi ya vituo vya kuwasajili wapiga kura.

Na hii imezua hofu kubwa miongoni mwa wapiga kura kuhusu uhakika wa mitambo hiyo wakati was uchaguzi mkuu utakaoandaliwa mwezi wa tatu mwakani.

Mwandishi: Eric Ponda/DW Mombasa
Mhariri: Mohammed Khelef