1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya amani ya maonyesho ya vitabu ya Frankfurt

Lillian Urio
24 Oktoba 2005

Bwana Orhan Pamuk, mwandishi wa vitabu kutoka Uturuki, ameshinda tuzo ya amani katika maonyesho ya vitabu mjini Frankfurt, Ujerumani. Kwa mujibu wa kamati iliyotoa tuzo hiyo, kitabu cha Bwana Pamuk kinaleta matumaini kwamba Ulaya na nchi ya Kiislam ya Uturuki, zinaweza kuwa na urafiki wa karibu.

https://p.dw.com/p/CHeX
Bwana Orhan Pamuk, mwandishi wa vitabu
Bwana Orhan Pamuk, mwandishi wa vitabuPicha: AP

Katika hutuba yake ya kupokea tuzo hiyo Bwana Pamuk alizikosoa nchi za Ulaya pamoja na nchi yake ya Uturuki.

Alitumia wakati huo kutoa wito wake kwa pande zote kutafuta njia ya kuelewana na kushirikiana.

Pia amekuwa akikampeni kwa muda mrefu sasa ili Uturuki ipate wanachama wa Umoja wa Ulaya, na katika hutuba yake alizungumzia tena juu ya suala hilo.

Bwana Pamuk anaikosoa Ujerumani kwa kusambaza hofu juu ya Uturuki kujiunga na Umoja huo. Amesema hofu hiyo ilisambazwa tena wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani, zilizofanyika mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Bwana Pamuk wanasiasa wa Ujerumani kusambaza hali ya wasiwasi juu ya Uturuki ni sawa na wanasiasa wa Uturuki wanyvokuwa wanaipinga Ulaya kwa jazba.

Bwana Pamuk anasema kama nchi za Ulaya zinajenga chuki dhidi ya Uturuki, basi nchini Uturuki nao watajenga chuki dhidi ya Ulaya na kuendeleza hisia za kitaifa.

Bwana Pamuk amekuwa akiandika kuhusu suala hili katika vitabu vyake. Suala hili la mgawanyiko wa mawazo baina ya pandehizo linaonekana wazi katika kitabu chake kinachoitwa ‘Schnee’, yaani Barafu ya theluji.

Kitabu hicho kinaelezea juu ya wahusika wenye misimamo tofauti sana, wanaoishi katika mji mdogo nchini Uturuki. Mada zinazojitokeza ni pamoja na fikira za wasomi wa nchi za magharibi, waislamu wenye siasa kali, wanawake wanaunga na kupinga uvaaji wa hijab na suala la hisia za kitaifa.

Kitabu hiki kimeweza kuwapa watu wengi wa nchi za Ulaya Magharibi hali halisi ya maisha ya Waturuki nchini mwao.

Bwana Joachim Sartorius, mkurugenzi wa tamasha la sanaa la mji wa Berlin, ni mpenzi wa vitabu vya Bwana Pamuk na amewahi kuishi Uturuki kwa kipindi cha miaka mitatu.

Bwana Sartorius ana mawazo yafuatayo kuhusu kazi ya Bwana Pamuk:

“Ni bahati kwetu kuwa kazi ya Bwana Orhan Pamuk inatuelezea juu ya nchi yake. Inazungumzia na kutueleza kuhusu masuala mengi, yakiwemo ya kisiasa, kijeshi na kihistoria. Mwandishi huyu ndiye wa pekee anayetuwezesha kuielewa nchi hii”.

Kwa mujibu wa Bwana Pamuk Waturuki wanataka kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa sababu wanadhani itamaanisha ongezeko katika usalama wa nchi yao na pia itaimarisha siasa katika Umoja huo.

Bwana Pumak anasema kwamba anayeamini kuwepo kwa Umoja wa Ulaya ni lazima aelewe suala hili ni kati ya amani na hisia za kitaifa. Ni lazima wachague kati ya amani au hisia za taifa.

Anaamini kwamba msingi wa Umoja huo ni amani na suala la Uturuki kutaka amani kati yake na Umoja huo lisipuuziwe.

Bwana Pamuk aliongeza kwamba itabidi watu wachague kati ya kazi za vitabu vya kubuni zinazohusu amani au hisia za kitaifa, zinazowafanya wachome moto vitabu hivyo.