1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia: Mvutano mkubwa baada ya rais kulisimamisha bunge

Zainab Aziz Mhariri: Jacob Safari
26 Julai 2021

Uamuzi wa Rais wa Tunisia Kais Saied wa kulisimamisha bunge na kumng'oa madarakani waziri wake mkuu umesababisha maandamano nchini humo. Serikali za kigeni zimeonyesha wasiwasi.

https://p.dw.com/p/3y5FN
Tunesien Krise l Entmachtung des Ministerpräsidenten, Soldaten umstellen Parlament
Picha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Ujerumani imeelezea wasiwasi wake juu ya hali ya nchini Tunisia. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, Maria Adebahr amewaambia waandishi wa habari kuwa Ujerumani inatumai kwamba Tunisia itarejea haraka kwenye utaratibu wa kikatiba.

Adebahr amefahamisha kwamba Ujerumani itajadili hali ya Tunisia na balozi wa nchi hiyo mjini Berlin. Amesisitiza kwamba demokrasia ilikita mizizi nchini Tunisia tangu mwaka 2011 baada ya maandamano ya kusaka mageuzi yaliyomwangusha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali. Umoja wa Ulaya umezitaka pande zote nchíni Tunisia kuheshimu katiba.

Msemaji wa ikulu ya Urusi, Dmitri Peskov, amesema nchi hiyo inafuatilia kwa makini kinachoendelea huko Tunisia. Amewaambia waandishi wa habari kwamba wana matumaini kuwa utulivu na usalama wa watu wa Tunisia hautatumbukizwa hatarini. 

Maafisa wa usalama nchini Tunisia wakikabiliana na waandamanaji nje ya Bunge
Maafisa wa usalama nchini Tunisia wakikabiliana na waandamanaji nje ya BungePicha: Fethi Belaid/AFP

Uturuki imesema inapinga kusimamishwa kwa mchakato wa kidemokrasia nchini Tunisia. Uturuki imelaani hatua zilizochukuliwa nchini Tunisia na imesema hazina uhalali wa kikatiba na kwamba haziungwi mkono na umma. Qatar imezihimiza pande zote kuepuka migogoro na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Hali ya wasiwasi imetanda nchini Tunisia huku jeshi likiamriwa kuingia barabarani ili kutuliza vurugu. Wakati huo huo wanasheria wanapingana na kutoa maoni tofauti kuhusu katiba ya Tunisia.

Baada ya rais Kais Saied kutoa taarifa ya kumfukuza waziri wake mkuu Hicham Mechichi na kutangaza kuwa atashika hatamu za mhimili wa utendaji na kushirikiana na waziri mkuu mpya atakaemteua, hatua yake hiyo ilijibiwa na kiongozi wa chama chenye wabunge wengi zaidi cha Ennahda, Rached Ghannouchi ambaye pia ni Spika wa bunge kwa kukaa mbele ya bunge kuashiria upinzani dhidi ya uamuzi wa rais.

Kushoto waziri mkuu aliyefukuzwa Hichem Mechichi. Kulia: Rais wa Tunisia Kais Saied.
Kushoto waziri mkuu aliyefukuzwa Hichem Mechichi. Kulia: Rais wa Tunisia Kais Saied.Picha: Slim Abid/AP Photo/picture alliance

Ghannouchi mwenye umri wa miaka 80 alizuiwa na jeshi kuingia bungeni. Wafuasi wa chama hicho cha Ennahda chenye sera za wastani za kiislamu na wale wa chama cha rais Saied walishambuliana kwa mawe nje ya bunge mapema leo. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanji na wengine wao wamekamatwa.

Matatizo ya muda mrefu yanayotokana na ukosefu wa ajira pamoja na kudorora kwa utendaji kazi wa serikali ndiyo maswala yaliyochochea maandamano ya kuipinga serikali nchini Tunisia.

Pamoja na nakisi katika bajeti, Tunisia inakabiliwa na matatizo ya kulipa madeni yake. Huenda nchi hiyo ikalamizika kutafuta mkopo mwingine kutoka shirika la fedha la IMF ambao unaweza kutifua matatizo mengine.

Vyanzo:/AFP/RTRE