1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Zimbabwe yasubiriwa kutangaza mshindi

Oumilkheir Hamidou
31 Julai 2018

Wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe wamesema wana matumaini ya kushinda

https://p.dw.com/p/32OZH
Simbabwe Wahl Auszählung
Picha: Gettey Images/AFP/M. Longari

Kila mmoja kati ya wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais nchini Zimbabwe, rais wa Emmerson Mnangagwa na mpinzani wake mkuu, kiongozi wa vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasia MDC Nelson Chamisa anajinata na kusema ana matumaini ya kushinda uchaguzi wa kwanza huru kuwahi kuitishwa baada ya miongo minne ya utawala wa Robert Mugabe.

Rais Emmerson Mnangagwa anasema chama chake tawala ZANU-PF kinapokea ripoti za "kutia moyo mno" huku kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa akisema chama chake cha MDC "kinafanya vizuri sana."

Madai hayo yanaashiria uwezekano wa kutiwa ila matokeo ya uchaguzi huo wa kihistoria na kuitishwa duru ya pili ya uchauzi mwezi wa september unaokuja ikiwa hakuna mgombea aliyejipatia angalao asili mia 50 ya kura.

Wagombea wawili wakuu. Kushoto ni Rais Emmerson Mnangagwa na kulia ni kiongozi mkuu wa upinzani Nelson Chamisa
Wagombea wawili wakuu. Kushoto ni Rais Emmerson Mnangagwa na kulia ni kiongozi mkuu wa upinzani Nelson ChamisaPicha: picture-alliance/AP Photo

Wanadiplomasia wa magharibi na wasimamizi wa ndani wanasema kinyang'anyiro hicho kilichowateremsha vituoni asili mia 75 ya wapiga kura, matokeo yake yanabanana mno.

Tume ya uchaguzi ZEC imesema hakujakuwa na visa vya udanganyifu wala wizi wa kura. Hata hivyo mtandao wa wasimamizi  wa Zimbabwe ZESN wamesema kumekuwa na shaka shaka kama tume ya uchaguzi inaweza kweli kuendesha shughuli zake kwa njia huru. Katika ripoti yake ya awali hata hivyo ZESN wali zoezi la auchaguzi limeandaliwa vyema ikilinganishwa na miaka iliyopita

Chama cha ZANU-PF kimekuwa kikiitawala Zimbabwe tangu uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 na ushindi wa upande wa upinzani unaweza kuzusha vurugu. Wadadisi wanasema haijulikani kama majenerali waliomng'owa madarakani Mugabe  mwaka jana na kumkabidhi hatamu za uongozi Mnangagwa, wataridhia ushindi wa Vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasi MDC.

Simbabwe Wahl Auszählung
Picha: Gettey Images/AFP/M. Longari

Chama tawala kikishindwa itakuwa sawa na kushindwa utawala wa Mnangagwa na kuna uwezekano jeshi likaingilia kati .

 Maafisa wa vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasia MDC wanasemekana wanatuma malalamiko kortini kuitaka tume ya uchaguzi ZEC itangaze matokeo yote.

"Nna wasi wasi kusije kukat0okea maachafuko" anasema Stone Sibanda, dereva mjini Harare anaeongeza kusema kila mtu ameingiwa na wasi wasi nchini humo.

Tume ya uchaguzi ZEC inatarajiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wakati wowote kutoka sasa. Dazeni kadhaa ya wafuasi wa upande wa upinzani MDC wameshaanza kukusanyika katika makao makuu ya chama chao na kusherehekea kilre wanachokiita ushindi wao.Kwengineko lakini mjini Harare hali ni shuwari.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga