1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Congo yaahirisha kutoa matokeo

Sekione Kitojo
6 Januari 2019

Tume ya uchaguzi ya DRCongo imechelewesha kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais,huku kukiwa ongezeko la mbinyo kutoka mataifa yenye nguvu na kanisa Katoliki kuheshimu matakwa ya wapiga kura.

https://p.dw.com/p/3B5F3
Kollage von den vier Top-Kandidaten DR Kongo

Matokeo ya  awali, ambayo  yalipangwa kutolewa  leo Jumapili, sasa yatatolewa  wiki  ijayo, mkuu  wa  tume  ya  uchaguzi  nchini  humo CENI ameliambia  shirika  la  habari  la  AFP masaa  machache kabla  ya  muda  wa  mwisho  kumalizika.

"Haitawezekana  kutangaza  matokeo  siku  ya  Jumapili. Tunapinga hatua , lakini  hatuna  kila  kitu bado," alisema Corneille Nangaa, bila ya  kutangaza  siku ya kutangaza  matokeo hayo.

Demokratische Republik Kongo - Wahl: Corneille Nangaa Yobeluo
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Corneille NangaaPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

Baraza  la maaskofu  wa  Kanisa  Katoliki  lenye ushawishi  mkubwa nchini  Congo , CENCO, ambalo  linawakilisha  maaskofu  wa Kikatoliki  nchini  humo , limeonya  kwamba  hasira za umma zinaweza  kujitokeza iwapo matokeo  ya  mwisho hayatakuwa  ya "kweli kwa mujibu wa matokeo halisi  ya  kura."

Kanisa linamjua mshindi

Kanisa katoliki  lenye ushawishi nchini  Congo, ambalo limetoa  zaidi ya  wachunguzi  wa  uchaguzi  40,000 , lilisema  siku  ya  Alhamis kwamba  linamjua mshindi  wa  uchaguzi  huo , lakini  halikumtaja.

Katika  barua  kwa  Nangaa  siku  ya  Jumamosi, rais  wa  baraza hilo  la  CENCO Marcel Utembi amesema  kwamba , kutokana  na uchelewesho  huo, "Iwapo  kutakuwa  na  vuguvugu  la  maandamano ya  umma  itakuwa  ni  jukumu  la  CENI."

Präsidentschaftskandidat der Demokratischen Republik Kongo, Martin Fayulu
Mgombea wa upinzani Martin FayuluPicha: Getty Images/A. Huguet

Uchaguzi  huo  wa  Desemba 30 ulishuhudia wagombea  21 wakipambana  kuwania  kuchukua  nafasi  ya  rais Joseph  Kabila , ambaye  ameitawala  nchi  hiyo kubwa , iliyokumbwa  na  mizozo kwa karibu miaka  18.

Miongoni  mwa wale  walioko  katika  nafasi  za  mbele ni  pamoja  na mrithi  aliyeteuliwa  na  Kabila Emmanuel Ramazani Shadary  na wagombea  wawili  wa  upinzani, mwanasiasa wa siku  nyingi mwenye  ushawishi  mkubwa Felix Tshisekedi  na Martin Fayulu ambaye  amejitokeza  hivi  karibuni.

DRCongo haijabadilisha kiongozi kwa amani

Anayetafutwa  ni mwanasiasa kiongozi  katika  nchi  hiyo  yenye utajiri  mkubwa  wa  madini  ambayo  haijawahi  kuwa na kipindi  cha madadiliko  ya  amani  ya  utawala  tangu  nchi  hiyo  kujipatia  uhuru kutoka  Ubelgiji  mwaka  1960.

Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Mgombea katika uchaguzi wa DRCongo Felix Tshisekedi akipiga kura yake mjini Kinshasa ,Desemba 30, 2019.Picha: Reuters/O. Acland

Kabila alikuwa  aondoke  madarakani  miaka  miwili  iliyopita, lakini aling'ang'ania  madarakani, na  kuzusha  maandamano  ya  umma ambayo  yalikandamizwa kikatili, na  kuuwa  watu  kadhaa.

Uchaguzi, ambao  ulitanguliwa  na  kucheleweshwa  mara  kwa mara, ulifanyika   katika  hali  ya  utulivu. Lakini  hali  ya  wasi  wasi imejijenga  katika  muda  wa  kipindi  cha  mchakato  wa  kuhesabu kura, huku  kukiwa  na  hofu  kwamba  matokeo  yanaweza kuchakachuliwa  ili  kumuweka Shadary  madarakani ambaye anaungwa  mkono  na Kabila.

Wahlen im Kongo
Emmanuel Ramazani Shadary akipiga kura katika uchaguzi wa Desemba 30 nchini DRCongoPicha: picture-alliance/AP/J. Delay

Tume  ya  uchaguzi  iliahidi  kutangaza  matokeo  ya  awali Jumapili (06.01.2019), na kufuatiwa na  tangazo  rasmi  la  matokeo  ya uchaguzi  hapo Januari  15.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Jacob Safari Bomani