1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya kusikiliza ushahidi yaundwa Uengereza

Oumilkher Hamidou24 Novemba 2009

Waengereza wataka kujua kama kuingia vitani Iraq ílikua halali

https://p.dw.com/p/KeM8
Mkuu wa tume ya uchunguzi wa vita vya Irak-John ChilcotPicha: picture alliance / empics

Tume ya uchunguzi iliyoundwa na waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown imeanza hii leo kusikiliza ushahidi kuhusu mchango wa Uengereza katika kuingia vitani nchini Iraq mnamo mwaka 2003 pamoja na madai ya udanganyifu ya ripoti za idara za upelelezi.

Huu ni uchunguzi wa tatu kufanywa kuhusiana na kadhia hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nchini Uingereza.

Uchunguzi wa tume hiyo inayoongozwa na John Chilcot utadumu miezi kadhaa na unaweza kukigeukia chama cha Labour wakati huu ambapo uchaguzi wa bunge huenda pengine ukaitishwa mwezi June mwakani.

Hata hivyo tume hiyo haitotangaza matokeo ya uchunguzi wake kabla ya mwisho wa mwaka 2010.

Tume hiyo ya watu watano,wote wakiwa wamechaguliwa na waziri mkuu Gordon Brown itajaribu kutathmini yote yaliyotokea,kwa kuwahoji wakuu wa kijeshi na wa idara za upelelezi na kuanzia mapema mwakani,kuwahoji pia wanachama wa serikali wa wakati ule,ikiwa ni pamoja na waziri mkuu Tony Blair.

"Tunataka kuelewa kwa uwazi kabisa,sababu tofauti zilizopelekea Uengereza kuingia vitani nchini Iraq-amesema John Chilcot,afisa wa ngazi ya juu wa zamani,alipokua akifungua shughuli za tume yake.

Amehakikisha watafanya kazi yao kikamilifu,bila ya mapendeleo na kwa njia za haki.Amekataa hata hivyo kuilinganisha tume yake na mahakama.

Hakuna yeyote anaefunguliwa mashtaka.Hatukuja hapa kusema nani ni mkosa na nani hana hatia amesisitiza mkuu wa tume hiyo John Chilcot.

Kabla ya tume hiyo kuanza shughuli zake John Chilcot aliiambia BBC

"Tumedhamiria kikamilifu kuandika kisa hichi kikamilifu na kwa dhati kutokana na misingi ya ushahidi tutakaoupata."

Sababu za kushiriki vitani Uengereza kwa ushirikiano pamoja na Marekani mnamo mwaka 2003 ndio kiini cha shughuli za kamisheni hiyo.

Uamuzi wa kutumwa wanajeshi 45 elfu wa Uingereza ulikua ukizidi kukosolewa kila miaka ilipozidi kupita nchini Uingereza.

Katika vikao vya maandalizi vya tume hiyo,familia za wanajeshi wa Uingereza waliouliwa nchini Iraq zilimlaumu Tony Blair wakati ule akiwa bado waziri mkuu,kutaka kuitosa Uingereza katika bahari ya vita kinyume na sheria na kuwahadaa waingereza kuhusu sababu za kuanzisha vita hivyo.

Serikali ya Uengereza wakati ule ilihalalisha uamuzi wake kwa hoja kwamba Sadam Hussein anamiliki silaha za maangamizi ya uma,silaha ambazo mpaka leo hata dalili yake haikuonekana.

Jumla ya wanajeshi 179 wa Uingereza wamepoteza maisha yao vitani nchini Iraq.Familia za wanajeshi hao zinataka tume ishughulikie mamabo matatu:kama vita vya Irak vilikua halali,kama zana za kijeshi zilikua za kufaa na kama ripoti za idara za upelelezi kuhalalisha kuingia vitani ni sahihi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Reuters)

Mhariri:Abdul Rahman