Tuhuma dhidi ya Rais Bashir zazua hisia tofauti | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 15.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Tuhuma dhidi ya Rais Bashir zazua hisia tofauti

Hatua ya kumshtaki rasmi Rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir kwa madai ya kuendesha kampeni ya mauaji ya halaiki pamoja na uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur imezua hisia tofauti katika jamii ya kimataifa

Luis Moreno-Ocampo mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC

Luis Moreno-Ocampo mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC

Mataifa ya magharibi yakiongozwa na Marekani ,Uingereza na Ufaransa yanataka kiongozi huyo ashtakiwe ila Uchina na Urusi walio na uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Sudan wanapinga vikali hatua hiyo.


Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC Louis Moreno Ocampo hapo jana aliwasilisha ushahidi uliothibitisha kuwa Rais Omar al Bashir alihusika na vitendo hivyo.Ushahidi huo unatolewa miaka mitatu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kumuagiza Bwana Ocampo kufanya uchunguzi wa madai hayo.

Majaji 18 wa mahakama hiyo ya kimataifa wanaowakilisha maeneo tofauti ya ulimwengu wanapaswa kutathmini ushahidi huo na kutoa uamuzi utakaoidhinisha au kupinga hatua ya kutolewa hati ya kukamatwa kwa Rais al Bashir.

Shughuli hiyo huenda ikachukua miezi kadhaa na imegubikwa na mazingira magumu ya kisiasa vilevile uwezekano wa kukamatwa kwa kiongozi wa nchi kutoka bara la Afrika aliye madarakani.Mmoja ya waendesha mashtaka anaeleza kinachoendelea


''Tumekuwa tukifanya uchunguzi na kwa mujibu wa ushahidi tulionao tutauwasilisha kwa majaji na wao ndio watakaofanya uamuzi.''Kwa mujibu wa ibara ya 16 ya Roma iliyoidhinisha kuanzishwa kwa mahakama hiyo,Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililo na wanachama 15 lina uwezo wa kuzuia hatua ya kumshtaki rasmi Rais Omar al Bashir.

Endapo mahakama hiyo itaamua kutoa hati ya kukamatwa kwa rais wa Sudan,juhudi za kusaka amani nchini humo huenda zikasambaratika.Hilo linaweza kuathiri hatma na operesheni za kikosi cha Umoja wa Mataifa na Afrika UNAMID kinacholinda amani kwenye eneo la Darfur.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye amekuwa akihusika kwa karibu na juhudi za kudumisha amani nchini Sudan anasisitiza kuwa mahakama hiyo ya kimataifa ni taasisi inayojitegemea na Umoja wa Mataifa sharti uheshimu hatua za kisheria inazochukua.


Kulingana na taarifa yake iliyotolewa Ijumaa iliyopita Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika linaeleza kuwa juhudi za kudumisha haki sharti zizingatie harakati za kutafuta amani ya kudumu.Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Jakaya Mrisho Kikwete alionya kuwa ghasia huenda zikatokea nchini humo endapo Rais Omar al Bashir atashtakiwa rasmi.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania Bernard Membe aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa niaba yake.


Serikali ya Sudan kwa upande wake imetoa wito wa kufanyika kwa kikao cha dharura cha mataifa wanachama wa Umoja wa nchi za Kiarabu.Sudan ni mwanachama wa jumuiya hiyo.Nchi hiyo inapinga vikali hatua hiyo dhidi ya kiongozi wake.


Kwa upande mwingine Umoja wa mataifa umetoa wito kwa Sudan kuhakikisha usalama kwa wafanyikazi wake.Sudan kwa upande wake imeahidi kutoa usalama kwa wafanyikazi wa Umoja huo vile vile kuunga mkono juhudi za kutafuta amani katika eneo la Darfur.Itakumbukwa kuwa Sudan si sehemu ya makubaliano ya mahakama ya ICC na imesema kuwa haitashirikiana na mahakama hiyo.


Hata hivyo Sudan ina wajibu wa kutimiza maombi ya mahakama ya kimataifa ya ICC kuhusiana na suala la uchunguzi katika eneo la Darfur.Endapo hati ya kukamatwa itatolewa na Sudan haitoridhia kutimiza ombi hilo Rais Omar al Bashir anaweza kukamatwa katika moja ya nchini yoyote iliyoidhinisha makubaliano ya kuunda mahakama hiyo ya ICC.Kwa sasa ni mataifa 106 yaliyoidhinisha suala hilo.


Chini ya mkataba uliopo majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa mataifa nchini Sudan hayana idhini ya kumkamata Rais Bashir endapo hati ya kukamatwa kwake itaidhinishwa.

Majeshi hayo hayatia juhudi zozote kuwakamata raia wengine wawili wa Sudan walioshtakiwa rasmi na mahakama hiyo ya ICC.


Kwa upande mwingine mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaunga mkono hatua hiyo japo wadadisi wanaonya kuwa kesi hiyo huenda ikachukua muda mrefu kabla kusikilizwa mahakamani.


 • Tarehe 15.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eciy
 • Tarehe 15.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Eciy
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com