Tsvangirai ataka Afrika imshinikize Rais Robert Mugabe | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 23.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Tsvangirai ataka Afrika imshinikize Rais Robert Mugabe

Kiongozi wa upinzani Zimbabwe Morgan Tsvangirai ataka Afrika kumshinikiza Rais Robert Mugabe wakati jumuiya ya kimataifa ikija juu kufuatia uamuzi wa kiongozi huyo kujitowa katika marudio ya uchaguzi wa urais.

Morgan Tsvangirai kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe akielezea uamuzi wake wa kujitowa marudio ya uchaguzi wa rais mjini Harare tarehe 22 mwezi wa Juni.

Morgan Tsvangirai kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe akielezea uamuzi wake wa kujitowa marudio ya uchaguzi wa rais mjini Harare tarehe 22 mwezi wa Juni.

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ataihimza Afrika wiki hii kuweka shinikizo kwa Rais Robert Mugabe kutatuwa mzozo wa kisiasa nchini humo baada ya kujitowa katika marudio ya uchaguzi wa rais.

Chama cha upinzani cha MDC kimesema rais wa chama hicho Tsvangirai katika siku mbili zinazokuja atauelezea uamuzi wao huo kwa dunia na kuzishawishi jumuiya za kimataifa hususan jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC na Umoja wa Afrika kuushinikiza utawala wa Mugabe kutatuwa mzozo wanaokabiliana nao.

Tsvangirai alijitowa katika marudio ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Ijumaa kwa kusema kwamba wafuasi wake watakuwa wanayahatarisha maisha yao iwapo watapiga kura.

Akizungumza masaa machache baada ya chama chake cha MDC kuripoti hapo jana kwamba mkutano wake wa hadhara umevunjwa na wafuasi wa Mugabe Tsvangirai amewaambia waandishi wa habari kwamba chama chake kimeamuwa kutoshiriki tena mchakato wa uchaguzi wa umwagaji damu usio halali na wa unafiki ambao matokeo yake tayari yamepangwa na Mugabe.

Amesema hawatomhalalisha Mugabe, hatutomruhusu kuwafanya wapumbavu wananchi wa Zimbabwe na jumuiya ya kimataifa na hawatocheza mchezo anaotaka Mugabe wacheze.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Havier Solana amesema uamuzi wa kiongozi huyo wa upinzani kujitowa katika marudio ya uchaguzi huo wa rais ni suala linaloeleweka na ameuelezea uchaguzi huo kuwa sawa na kuikejeli demokrasia.

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiita hatua hiyo ya Tsvangirai kuwa ya kusikitisha sana na mkosi kwa mustakablai wa taifa hilo Marekani imesema italifikisha suala hilo la Zimbabwe kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na imeitaka serikali ya Zimbabwe na wahuni wake kukomesha mara moja umwagaji damu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeir amesema kujitowa kwa Tsvangirai katika marudio hayo ya uchaguzi ni pigo kwa nchi hiyo na eneo zima la kusini mwa Afrika.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Miliband anaamini kwamba wamefikia kipindi muhimu sana kwa wananchi wa Zimbabwe kuondokana na utawala wa kikatili wa Robert Mugabe.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amesema atawashajiisha Mugabe na Tsvangirai kuujadili mzozo huo wa kisiasa na Rais Levy Mwanawaswa wa Zambia mwenyekiti Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC amesema uchaguzi huru na wa haki hauwezi kufanyika Zimbabwe na ametaka uchaguzi huo uhairishwe kuepeusha balaa katika eneo hilo.

Wakati jumuiya ya kimataifa ikichemka serikali ya Zimbabwe imesema uchaguzi huo utaendelea kufanyika kama ilivyopangwa.

Sikanyiso Ndlovu waziri wa habari wa Zimbabwe amesema uchaguzi utafanyika na wanaendelea mbele kwa kuwa hiyo ni mamlaka ya kikatiba na sio marudio ya uchaguzi wa Tsvangirai au marudio ya uchaguzi wa Uingereza.Hiyo ni katiba ya Zimbabwe ambayo inataja iwapo wagombea wanashindwa kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura kunapaswa kuwepo kwa marudio ya uchaguzi.

Chama cha upinzani kinasema helikopta za kijeshi zimekuwa zikipiga doria juu ya mji wa Harare na Bulawayo mji wa pili kwa ukubwa na kwamba Zimbabwe kwa kweli iko chini ya utawala wa kijeshi.

 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EOeO
 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EOeO
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com