1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras atafuta kuungwa mkono nyumbani

Admin.WagnerD16 Juni 2015

Waziri mkuu wa Uigiriki Alexis Tsipras leo anatafuta uungaji mkono kwa serikali yake nyumbani, katika vuta nikuvute inayoendelea kati yake na wakopeshaji juu ya makubaliano ya kuiokoa nchi hiyo isifilisike.

https://p.dw.com/p/1Fhsv
Griechenland - Alexis Tsipras spricht im Parlament
Picha: REUTERS/Alkis Konstantinidis

Tsipras alikutana Jumanne na mwanasiasa wa juu a chama cha kihafidhina pamoja na viongozi wa vya vya kisoshalisti na vile vinavyouunga mkono Umoja wa Ulaya, wakati ambapo Ugiriki ikizidi kukabiliwa na mbinyo kutoa tahfifu, na kukiwa hakuna mapendekezo mapya kutoka upande huo.

Serikali ya mrengo mkali wa kushoto mjini Athens inapinga miito kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa kupandisha kodi na kupunguza malipo ya pensheni, ikihoji kuwa hatua kama hizo tayari zimeshindwa kuufufua uchumi wa Ugiriki ulizorota vibaya.

Mpango wa Umoja wa Ulaya na IMF wa kuiokoa Ugiriki unamalizika muda wake Juni 30, na ilitarajiwa kuwa makubaliano yangekuwa yamefikiwa kufikia siku ya Alhamisi wakati wa mkutano wa mawaziri 19 wa kanda inayotumia sarafu ya euro mjini Luxembourg.

Waziri mkuu Tsipras na waziri wake wa fedha Yanis Varoufakis.Athen
Waziri mkuu Tsipras na waziri wake wa fedha Yanis Varoufakis.Picha: L. Gouliamaki/AFP/Getty Images

Pia mwishoni mwa mwezi huu, Ugiriki inatakiwa kulipa euro bilioni 1.6 kwa IMF, huku kiasi kingine cha euro bilioni 6.7 kikitakiwa kulipwa kwa Benki kuu ya Ulaya mwezi Julai na Agosti, malipo ambayo maafisa wa Ugiriki wanasema serikali haiwezi kuyamudu.

Hakuna mapendekezo mapya kwa kundi la Euro

Lakini waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amesema leo kuwa serikali mjini Athens haitopeleka orodha mpya ya mapendekezo ya mageuzi kwa mkutano wa Luxembourg.

Varoufakis aliliambia gazeti linaloongoza kwa mauzo nchini Ujerumani la Bild, kwamba mkutano wa mawaziri hao maarufu kama Kundi la Euro, siyo mahala sahihi pa kuwasilisha mapendekezo ambayo hayajajadiliwa kwa ngazi ya chini.

Lakini alisema timu ya majadiliano ya nchi yake ipo tayari wakati wowote kutafuta suluhu ya muafaka na washirika wake, kwa sharti kuwa wawakilishi wao wanakuja kwenye meza ya mazungumzo wakiwa na mamlaka thabiti na iliyo bayana.

Wahafidhina waahidi kuunga mkono makubaliano

Kiongozi wa chama cha siasa za mrengo wa kati cha To Potami Stavros Theodorakis amemtolea mwito waziri mkuu Tsipras leo kufikia makubaliano na wakopeshaji, na kusema chama chake kiko tayari kuunga mkono bungeni, makubaliano yoyote yatakayoibakiza Ugiriki katika kanda ya euro.

Theodorakis amesema Tsipras aliamuambia bado kulikuwa na hatua mbili au tatu Athens inazoweza kuzichukuwa ili kuondoa mkwamo katika mazungumzo na wakopeshaji, ilimradi na wakopeshaji wanalegeza msimamo wao pia.

Waziri mkuu Tsipras akiwa na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker.
Waziri mkuu Tsipras akiwa na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker.Picha: Reuters

Lakini msemaji wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, alisema jana kuwa Umoja wa Ulaya na IMF zimeshatoa tahfifu kubwa tu kwa Ugiriki. Mazungumzo haya yanayolenga kufikia muafaka ili Ugiriki ipatiwe euro bilioni 7.2 zilizobakia kwenye mpango wa uokozi wa nchi hiyo yameendelea kwa muda wa miezi mitano sasa.

Kanda ya euro yaanda mpango wa dharura

Wakati huo huo,kwa mujibu wa gazeti la Süddeutsche Zeitung washirika wa Ugiriki katika kanda ya euro wanaandaa mpango wa dharura wa kukabiliana na kitisho cha machafuko ya kiuchumi nchini Ugiriki, ikiwa taifa hilo litashindwa kufikia makubaliano na wakopeshaji wiki hii.

Mpango huo unahusisha kuweka vidhibiti juu ya mitaji mwishoni mwa wiki, kuzuwia uwezekano wa benki za Ugiriki kuishiwa fedha.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe,rtre
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman.