Trump na Modi wasifu mahusiano ya Marekani na India | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump na Modi wasifu mahusiano ya Marekani na India

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wamefanya mkutano wao wa kwanza wa ambapo masuala ya biashara na ulinzi yalipewa kipau mbele.

Trump na Modi walikumbatiana kuonyesha kuwa wao ni marafiki na washirika, huku wakieleza kuwa dhamira yao ya ukuaji wa uchumi itaimarisha na sio kudhoofisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili makubwa duniani.

Wakati mahusiano ya Trump na baadhi ya washirika wa zamani wa Marekani yalianza kwa matatizo, yeye na Modi walionekana kuweka maelewano ya moja kwa moja katika mkutano wao wa kwanza, huku wakikumbatiana katika bustani ya Ikulu ya mjini Washington mbele ya wanahabari. "Nnatarajia kufanya kazi nawe Bwana Waziri Mkuu, kuweka nafasi za ajira katika nchi zetu, kuweka mazingira ya ukuaji wa uchumi na kuweka uhusiano wa kibiashara ambao ni wa haki na usawa. Ni muhimu kuondolewa vizuizi vya kuuza bidhaa katika masoko yenu na tupunguze pengo la kibiashara na nchi yako".

Modi alisema anataka kuuweka ushirikiano wa kimkakati kati ya Marekani na India kwenye viwango vipya "Tunaichukulia Marekani kuwa mshirika wa msingi kwa mabadilikio ya kijamii na kiuchumi nchini India na katika mipango yetu yote muhimu. Nna uhakika kuwa maono yangu ya India mpya na maono ya Trump ya kuifanya Marekani kuwa bora tena vitaweka mwelekeo mpya kwenye ushirikiano wetu".

USA Trump und Modi im Weißen Haus (Reuters/K. Lamarque)

Ulikuwa mkutano wa kwanza kati ya Trump na Modi

India kwa sasa ndilo taifa kubwa kabisa ulimwenguni linalokuwa kwa kasi kiuchumi, hadhi ambayo Modi anatumai kuitumia kwa kuvutia uwezekaji zaidi wa kigeni – kwa sehemu kwa kuhimiza makampuni ya utengenezaji bidhaa kufanya biashara katika nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa kiuchumi barani Asia.

Wachambuzi walikuwa wametabiri kuwa Trump na Modi wangekuwa na mambo mengi yanayofanana, ambapo viongozi hao wawili waliingia madarakani kwa kujionyesha kuwa watu waliokuwa nje ya ulingo wa kisiasa.

Tofauti zozote kuhusu masuala kama vile uhamiaji na mabadiliko ya tabia nchi yaliwekwa kando na badala yake waliahidi kushirikiana kwa karibu katika kupambana na ugaidi, vita nchini Afghanistan na ushirikiano wa ulinzi.

Kabla ya mazungumzo na Trump, Modi alikutana na Waziri wa Ulinzi Jim Mattis na Waziri wa Mambo ya Kigeni Rex Tillerson. Wizara ya mambo ya kigeni ilitangaza baadaye kuwa inamwekea vikwazo kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi linalopigania kujitenga la Hizb-ul-Mujahideen katika jimbo la Kashmir.

Usalama wa kikanda ulijumuishwa katika mazungumzo hayo, ikiwa ni pamoja na Afghanistan, wakati Marekani inazingatia kupeleka wanajeshi wa ziada hadi 5,000 kuwasaidia wanajeshi wa nchini humo kupambana na makundi ya uasi. Trump aliwashukuru watu wa India kwa mchango wao katika kusaidia maendeleo nchini Afghanistan.

Modi kwa upnde wake alisema India itaendelea kuwa na mashauriano na mawasiliano ya karibu na Marekani ili kutimiza lengo la pamoja la amani na utulivu. India kila mara huituhumu hasimu wake Pakistan kwa kuchochea machafuko nchini Afghanistan na kuyaficha makundi ya wanamgambo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com