1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na biashara siku 100 za kwanza madarakani

Iddi Ssessanga
29 Aprili 2017

Katika siku yake ya 100 madarakani Rais Donald Trump atazungumzia biashara katika mmoja ya majimbo yaliochangia ushindi wake usiotarajiwa, ambapo atasaini amri ya rais kutathmini upya mikataba ya biashara ya taifa hilo.

https://p.dw.com/p/2c71p
USA Präsident Donald Trump bei der NRA - National Rifle Association
Picha: Reuters/J. Ernst

Ni mmoja ya amri mbili ambazo rais huyo atazitia saini katika kiwanda cha koleo katika kaunti ya Cumberland jimboni Pennsylvania, aina ya eneo lililosukuma mbele ushindi wake wa kushangaza. Wiki iliopita ilishuhudia mhemuko mkubwa katika ikulu ya White House wakati Trump na timu yake wakijaribu kuorodhesha mafanikio na kutimiza ahadi kabla ya kufika siku ya kiishara ya 100.

Pamoja na ziara ya kiwanda cha zana cha Ames, ambacho kimekuwa kikitengeneza koleo tangu 1774, Rais Trump atafanya mkutano aina ya ile alioifanya wakati wa kampeni kuhitimisha siku hiyo. Ni kama kurudi kwenye kanuni kwa rais ambaye, katika siku za karibuni amekuwa akitoa matamshi yanayoashiria kutoridhika na mafanikio yake mpaka sasa.

Amri nyingi zaidi za rais katika siku 100

Mapema wiki hii, Trump alitangaza azma yake ya  kuujadili upya mkataba wa biashara huria wa mataifa ya Amerika Kaskazini (NAFTA). Alisema pia angeanza kujadili upya makubaliano ya biashara huria na Korea Kusini, ambayo kwake Marekani ina nakisi kubwa ya kibiashara. "Hakuna siku inayopita bila rais kuzungumzia suala la biashara," alisema waziri wa biashara Wilbur Ross akiwa ilkulu siku ya Ijumaa.

Großbritannien Protest von Amnesty International gegen 100 Tage Trump in London
Shirika la haki za binadamu la Amnesty International lilifanya maandamo mjini London tarehe 27.04.2017 wakiwa wamevalia kama mnara wa uhuru kupinga maadhimisho ya siku 100 za utawala wa Trump.Picha: picture-alliance/dpa/PA Wire/Yui Mok

Amri za rais zinazosainiwa siku ya Jumamosi zitakuwa ya 31 na 32 tangu alipoingia madarakani - idadi ambayo ndiyo kubwa zaidi kuwahi kusainiwa na rais katika siku 100 za kwanza madarakani tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia. Ni hali tofauti kabisaa na matamshi ya Trump alioyatoa wakati wa kampeni, alipomkosa mtangulizi wake kwa kutumia njia hiyo, ambayo ina faida ya kutohitaji idhini ya bunge.

Amri muhimu zaidi kati ya mbili itaipa wizara ya biashara na mwakilishi wa biashara wa Marekani siku 180 kubaini ukiukaji na matumizi mabaya chini ya mikataba ya biashara ya taifa hilo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Ross alisema shirika la biahara duniani WTO lina ukiritimba mwingi na limepitwa na wakati na linahitaji kufanyiwa mageuzi.

Waziri huyo wa biashara alipuuza uwezekano wa Marekani kujiondoa kwenye shirika hilo la usuluhishi wa sheria za biashara duniani lenye makao yake mjini Geneva, lakini hakuondoa uwezekano huo. "Kama ilivyo kwa shirika lolote la kimatifa, huwa kuna uwezkano wa kufanya marekebisho," alisema.

China bado yamuumiza kichwa

Utawala wa Trump unahoji kuwa ushindani usio wa haki na China na washirika wengine wa kibiashara umefuta mamilioni ya ajira za viwandani nchini Marekani. Ross alisema kutoridhirishwa na sera ya kibiasahra ndiyo mmoja ya sababu wapigakura walimgeukia Trump katika uchaguzi.

"Wamechoka kuona ajira zao zinahamia nje ya nchi. Wamechoshwa na baadhi ya matendo yanayoharibu," alisema. "Hivyo, kimsingi taifa lilisema katika uchaguzi uliopita: Ni wakati wa kurekebisha mambo. Na rais alisikia ujumbe huo."

Facebook Simpsons-Clip zu 100 Tage Trump
Trump amekuwa akitumia mitandao ya kijamii, hasa twita kuwasiliana katika siku zake 100 za kwanza madarakani. Katuni hii ya The Simpsons inaonyesha uraibu wa Trump linapokuja suala la twita.Picha: Facebook/The Simpsons

Trump ambaye aliahidi kuishughulikia China na washirika wengine wa kibiashara, ametangaza hatua kadhaa nyingine katika wiki za karibuni. Ameiaguza wizara ya biashara kuchunguza sababu za nakisi kubwa katika bishaa za kibiashara za Marekani iliyofikia dola bilioni 734 kwa mwaka uliopita, dola bilioni 347 zikiwa katika biashara na China pekee.

Utawala huo pia unaanza kuziwekea ushuru bidhaa za mbao laini kutoka Canada, na unachunguza iwapo bidhaa za nje za chuma na aluminium zinasababisha kitisho kwa usalama wa taifa. Robert Lighthizer, wakili wa biashara ambaye Trump amemteuwa kuwa mwakilishi wake wa biashara, amekosa uamuzi wa mwaka 2001 wa kuiruhusu China kujiunga na WTO.

Malalamiko dhidi ya WTO

Washington ilichukulia kwa kutojua, kwamba China ilikuwa "mfano tu wa nje wa Canada," Lighthiner aliwahi kuthibitisha, na kwamba ingejifunza kuishi ndani ya sheria za WTO na kufungua soko lake kwa bidhaa za Marekani; badala yake China imedhibiti ushindani wa nje, kuchezea thamani ya sarafu yake na kuwapatia ruzuku wafanyabiashara wake wa nje.

Ross alisema Ijumaa kuwa WTO imejielekeza zaidi kuhusu kudhibiti ushuru wa desturi - kodi kwenye bidhaa za nje - na halifanyi vya kutosha kukabiliana na vikwazo visivyo vya kidesturi vya biashara au kuzuwia ukiukaji wa haki za umiliki wa hataza.

Trump anashinikiza kuwepo na ruwaza ya makubaliano ya kibiashara ya kutendeana, ambamo Marekani inaweza kupandisha au kushusha ushuru kwa bidhaa za taifa kulingana na namna nchi hiyo inavyoitendea Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Sekione Kitojo