Trump kumkaribisha Rais wa Korea Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump kumkaribisha Rais wa Korea Kusini

Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in huenda wakawa na msimamo wa pamoja kuhusu Korea Kaskazini katika Ikulu ya White House hii leo na kesho. Suala la biashara pia litajadiliwa

Mvutano kuhusu biashara huenda ukaathiri juhudi zao za kuimarisha uhusiano wa Marekani na Korea Kusini. Moon, ambaye anafanya ziara yake ya kwanza nchini Marekani tangu alipochaguliwa kuwa kiongozi wa nchi yake, atajiunga na Trump na mkewe Melania, kwa chakula cha jioni katika Ikulu ya White House leo usiku kabla ya kufanya mikutano kesho Ijumaa ambayo inatarajiwa kugusia mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, jukumu la China katika kanda hiyo na mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora wa jeshi la Marekani maarufu kama THAAD.

Marais hao wawili wana nia ya kujenga uhusiano imara. Moon anataka kuunda urafiki na mfanyabiashara huyo wa zamani wa New York na kupata msimamo wa pamoja kuhusu mbinu za kuutatua mzozo wa Korea Kaskazini wa mipango ya nyuklia na makombora. Trump anataka kujenga mahusiano na kiongozi muhimu katika kanda hiyo wakati akiendelea kufadhaishwa na hatua ya China kushindwa kuingilia suala la Korea Kaskazini, licha ya uhusiano wake na Rais wa China Xi Jinping.

USA THAAD Raketenabwehrsystem (Getty Images/Lockheed Martin)

Mtambo wa THAAD wa kujikinga dhidi ya makombora

Suala la biashara huenda huenda likaathiri mchakato wa kujenga mahusiano. Katika mahojiano na shirika la habari la Reuters mwezi wa Aprili, trump aliuita mkataba wa biashara uliodumu miaka mitano kati ya Marekani na Korea Kusini maarufu kama KORUS, kuwa ni "mbaya sana” na "usiokubalika”, na akasema ataujadili upya au ausitishe. Afisa mmoja wa Ikulu ya White House amesema kuwa Trump na Moon watakuwa na mazungumzo ya wazi na kirafiki kuhusu mahusiano ya kibiashara.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Biashara la Marekani hapo jana, Moon alisema vitendo visivyo vya haki vya kibiashara vitaondolewa na sababu zinazodhibiti ushindani, kama vile vikwazo vya kupenya katika masoko na udhibiti wa bei, zitatathminiwa upya chini ya utawala wake.

Kumekuwapo na wasiwasi kuhusu vizingiti vya mauzo ya magari nchini Marekani na kiwango kikubwa cha chuma cha pua kutoka China ambacho huwasili Marekani kupitia Korea Kusini.

Suala jingine nyeti linalotazamiwa kuguswa katika mazungumzo hayo huenda likahusu mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora ambao Marekani iliweka nchini Korea Kusini mwezi Machi. Moon, ambaye anahimiza mtazamo wa wastani kuhusu Korea Kaskazini, alielezea kushutushwa kwake mwezi uliopita baada ya kufahamishwa kuwa mitambo minne zaidi ya mfumo huo tata wa makombora imeingizwa nchini mwake. Aliagiza uchunguzi baada ya Wizara yake ya Ulinzi kukosa kumfahamisha kuhusu hatua hiyo.

Mfumo huo, ambao kujengwa kwake kuliikarisisha China, unalenga kuzuia kitisho kutokana na mpango wa makombora wa Korea Kaskazini. Licha ya kuwako na mambo kadhaa ya mgongano, viongozi hao wawili wanatarajiwa kuelezea msimamo wa pamoja kuhusu vitisho kutoka kwa Korea Kaskazini.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com