Trump azindua mkakati wa usalama wa taifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump azindua mkakati wa usalama wa taifa

Rais wa Marekani, Donald Trump ametumia uzinduzi wa Mkakati wake wa Kwanza wa Usalama wa Taifa kuzisifu faida za ushirikiano wa nchi yake na Urusi,

Akizindua hati ambayo ilizishambulia Urusi na China kuwa "madola yanayorudisha nyuma maslahi ya wengine” ambayo yana nia ya kuyarudisha nyuma maslahi ya Marekani, Trump alisifu ushirikiano wa karibuni wa kupambana na ugaidi kati ya Urusi na Marekani.

Sauti yake ya maridhiano kwa Putin ni tofauti kabisa na hati hiyo ya mkakati yenye kurasa 68 ambayo ilitayarishwa na wasaidizi muhimu. Waraka huo unatumia lugha kali kuonyesha picha kuwa China na Urusi kuwa washindani wa kimataifa ikisema kuwa nchi hizo zinashindana na nguvu za Marekani, ushawishi, na maslahi, kujaribu kudhoofisha usalama wa Marekani na ustawi. Aidha, mkakati huo unaonya kuwa Urusi inalenga kudhoofisha ushawishi wa Marekani duniani na kuigawa nchi hiyo na washirika wake, wakati silaha za nyuklia za Urusi zikibakia kuwa kitisho kikubwa kabisa kwa Marekani.

Mkakati huo unaituhumu China kwa kutaka "kuiondoa Marekani” barani Asia, huku ukiorodhesha msururu wa malalamiko ya Marekani kuanzia mapungufu, wizi wa data hadi kwa kusambaza "sifa za mfumo wake wa kimabavu”.

Vietnam | APEC-Gipfel | Trump und Putin (REUTERS/Sputnik/Kremel/M. Klimentyev)

Putin alishukuru kupewa taarifa za CIA

Msemaji wa Ubalozi wa China amejibu vikali akisema "ni kitu cha kibinafsi sana kwa nchi kudai kuwa maslahi yake yenyewe ni bora zaidi kuliko maslahi ya nchi zingine na maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa”

Nakala hiyo ambayo imechukua miezi 11 kutayarishwa, inahitajika kisheria na hutengenezwa kwa ajili ya kuweka mfumo wa jinsi Marekani inaiuangalia ulimwengu. Mikakati ya awali ya usalama wa taifa ilizinduliwa bila kumulikwa sana katika vyombo vya habari na ilitumika kama miongozo, na sio amri za mafundisho. Lakini katika utawala wa Trump, hati hiyo imechukua umuhimu zaidi

Maafisa wa kigeni mjini Washington kila mara hulalamika kuwa kuna serikali mbili zinazofanya kazi, moja wanayoisikia katika mawasiliano ya kila siku na Wizara ya Mambo ya Kigeni na ya Ulinzi, na nyingine inayotoka kwa Trump, aghalabu kupitia mtandao wa kijamii Twitter.

Trump na washauri wake kila mara hutofautiana vikali kuhusu masuala muhimu ya usalama kuanzia Mashariki ya Kati hadi kwa mazungumzo na Korea Kaskazini. Lakini washirika wanaotaka ufafanuzi kuhusu nia ya dola hilo kubwa kiuchumi na kijeshi wanaweza kuchanganyikiwa na ujumbe wa mchanganyiko unaotoka kwa Trump.

Tangu alipoingia madarakani, Trump amejitahidi kuiondoa sifa ya mtangulizi wake Barack Obama kuanzia masuala ya mabadiliko ya tabianchi hadi biashara huru, mara nyingine kuiacha Marekani ikiwa imetengwa kwenye jukwaa la kimataifa. Hapo jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa wingi kuidhinisha azimio la kuukataa uamuzi wa karibuni wa Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, hatua ambayo Marekani ilipinga kwa kutumia kura yake ya turufu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com