1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amewasili Singapore kukutana na Kim

Josephat Charo
10 Juni 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amewasili Singapore leo (10.06.2018) kuhudhuria mkutano wa kihistoria na kiongozi wa Korea Kaskazaini, Kim Jong Un, kuhusu mustakbali wa silaha za nyuklia za taifa hilo la eneo la Korea.

https://p.dw.com/p/2zEuN
Singapur: U.S. Präsident Donald Trump bei der Ankunft
Picha: Reuters/ J. Ernst

Trump amewasili katika uwanja wa ndege wa jeshi la Singapore wa Paya Lebar akiwa katika ndege yake ya Air Force One, akitarajia kuweka msingi wa mkataba wa nyuklia na mojawapo ya mahasimu wabaya kabisa wa Marekani.

Trump amewasili Singapore akitokea Canada alikohudhuria mkutano wa kundi la mataifa yaliyostawi kiviwanda la G7. Baada ya safari ya saa 20 kutoka Canada, Trump alilakiwa katika uwanja wa ndege wa kijeshi na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Singapore Vivian Balakrishnan.

Trump amewasili saa chache baada ya Kim kutua Singapore katika ziara yake ndefu ya kigeni kama mkuu wa nchi. Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana siku ya Jumanne (12.06.2018) katika kisiwa cha mapumziko cha Sentosa kwa mkutano wa kilele unaowekewa matumaini makubwa; mazungumzo ya kwanza kati ya rais wa Marekani aliye madarakani na kiongozi wa Korea Kaskazini.

Miezi michache iliyopita mkutano kama huyo haungefikirika wakati Trump na Kim walipokuwa wakitupiana maneno ya matusi na vitisho vilivyoongeza hofu ya kutokea vita katika rasi ya Korea. Lakini mfululizo wa jitihada za kidiplomasia zilizoihusisha Korea Kaskazini, Korea Kusini na Marekani, zilipunguza hali ya wasiwasi na kumfanya Trump mwezi Machi kwa haraka kuukubali mualiko wa Kim kukutana naye.

Matarajio ya kupatikana makubaliano si makubwa

Awali Trump alifutilia mbali uwezekano wa kuafikia makubaliano makubwa na Korea Kaskazini ya kuusitisha mpango wake wa silaza zake na nyuklia ambao umepiga hatua kwa haraka kiasi cha kuitishia Marekani.

Singapur Kim Jong Un (l),  Lee Hsien Loong Premierminister
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, kushoto, na waziri mkuu wa Singapore, Lee Hsien LoongPicha: picture-alliance/dpa/Wong Maye-E

Trump amesisitiza atafaulu kukipata kile ambacho tawala zilizopita za Marekani zimeshindwa kukifanikisha.

Lakini tangia hapo amepunguza matarajio ya mkutano huo, akisema mazungumzo yake na Kim yatakuwa zaidi ya kuweka msingi wa mchakato wa mazungumzo utakaochukua zaidi ya mkutano mmoja wa kilele. Hii imejumuisha kuondokana na sharti la awali la Korea Kaskazini kuangamiza haraka silaza zake za nyuklia.

Trump alisema Alhamisi iliyopita kwamba hafikrii alilazimika kujiandaa sana kwa mkutano wake na Kim na kwamba kikao chao kinahusu zaidi mtizamo na hisia. Lakini maafisa kadhaa wa Marekani wamehoji iwapo Trump anachukua hatua za kutosha kuhakikisha anakwenda kwa kasi inayotakiwa.

Trump aliwaambia waandishi wa habari nchini Canada hapo jana kwamba makubaliano yoyote na Kim yatakuwa taarifa kubwa ya kusisimua, akisisitiza juu ya matokeo yasiyojulikana ya kile alichokiita "tume ya amani."

Mwandishi: Josephat Charo/reuters/afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid