Trump awasili Seoul na amwalika Kim Jong Un | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump awasili Seoul na amwalika Kim Jong Un

Trump yuko  nchini  Korea  kusini  kwa  ajili  ya  mikutano  na  rais Moon Jae In , baada  ya wote  kumaliza kuhudhuria  mkutano  wa  G20  nchini  Japan.

Rais wa Marekani Donald Trump amewasili Korea  kusini jioni jana  Jumamosi kwa matumaini ya  kukutana  na  kiongozi wa  Korea  kaskazini  Kim Jong Un  katika  kanda isiyokuwa  na  shughuli  za  kijeshi  DMZ , ambapo  viongozi  hao  wawili wanaweza  kupeana mikono  na  kusabahiana.

Trump alitoa  mwaliko kwa  mkutano  huo ambao  unaonekana  kuwa  ni  ghafla, mara  ya kwanza  katika  ukurasa wa  Twitter  na  kisha  mbele  ya  waandishi  habari  katika  mkutano wa  mataifa  tajiri  na  yale  yanayoinukia  kiuchumi  ya  G20 nchini  Japan, masaa kadhaa  tu kabla  ya  kuondoka  kwenda  katika  mji  mkuu  wa  Korea  kusini  katika  hatua  yake nyingine  ya  ziara yake.

"Iwapo mwenyekiti Kim wa  Korea  kaskazini  anaiona  hii, nitakutana  nae  katika  mpaka wa  eneo  hilo  lililotengwa  bila  shughuli  za  kijeshi ili  kumpa mkono  na  kusabahiana" Trump  aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter.

"Nilifikiria kuhusu  hilo  leo  asubuhi tu," Trump baadaye  aliwaambia  waandishi  habari. Nilitoa tu taarifa  fupi , kwasababu  sifahamu  yuko  wapi  hivi  sasa, huenda  hayuko  nchini Korea  kaskazini. Iwapo mwenyekiti Kim atapenda  kukutana , nitakuwa  katika  mpaka. Inaelekea  kunapata sana."

Naibu  wa  kwanza  wa  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa Korea kaskazini Choe Son Hui ameuita  mwaliko  huo, shauri linalofurahisha sana,"  lakini  amesema  anasubiri  pendekezo ambalo  ni  rasmi  zaidi, kwa  mujibu  wa  shirika  la  habari  la  Korea  kusini  Yonhap.

Endapo Trump na Kim watakutana, basi itakuwa mara ya tatu wanakutana ndani ya mwaka mmoja na miezi minne

Endapo Trump na Kim watakutana, basi itakuwa mara ya tatu wanakutana ndani ya mwaka mmoja na miezi minne

Iwapo  mkutano  huo  uliotayarishwa  kwa  haraka  katika  mpaka  kati ya  mataifa  hayo mawili  utafanyika, inawezekana  kuwa  kwa  dakika  mbili, kwakuwa  huo  ndio  muda ambao  utapatikana, Trump  alisema, akilifanya  tukio  hilo  kuwa  ni  fursa  tu  ya  kupiga picha.

Trump yuko  nchini  Korea  kusini  kwa  ajili  ya  mikutano  na  rais Moon Jae In , baada  ya wote  kumaliza kuhudhuria  mkutano  wa  G20  nchini  Japan. Trump  na  wafanyakazi  wa ikulu ya  White House, ikiwa  ni  pamoja  na  binti  yake  Ivanka Trump  na  mume wake  Jared Kushner , walilakiwa  Jumamosi  jioni  na  Moon  katika  Ikulu  ya  Blue House mjini  Seoul, eneo  la  ofisi  za  serikali  nchini  Korea  kusini  na  makao  ya  rais.

Trump  amekutana  mara  mbili  na  Kim , mara  ya  kwanza  mjini  Singapore  na  baadaye mjini  Hanoi, wakati  akijaribu  kuokoa makubaliano  yaliyoonekana  kuwa  ya  kihistoria kuifanya  Korea  kaskazini  kuachana  na  silaha  za  kinyuklia  ili  kuweza  kupata kuondolewa  vikwazo.

Mkutano  wa  Hanoi ulishindwa, na  kuzusha  wasi  wasi  kuwa  majadiliano hayo yamekwama  na  kwamba  hali  ya  wasi  wasi  inaweza  kuongezeka.