1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump avunja itifaki kwa kumpigia simu rais wa Taiwan

Bruce Amani
3 Desemba 2016

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amesababisha mzozo mwengine, baada ya kubainika kwamba alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen, na kuvunja itifaki nyengine ya kidiplomasia

https://p.dw.com/p/2Tfy2
Kombobild Trump und Tsai Ing-wen
Picha: Getty Images/T. Wright/A. Pon

Ni mazungumzo ya kwanza ya aina hiyo kutokea kati ya Marekani na Taiwan tokea mwaka 1979. Hadhi ya kisiwa hicho imekuwa kwa muda mrefu moja ya masuala yenye utata zaidi kati ya Marekani na China. Trump ameonyesha kukosa diplomasia katika masuala yanayoihusu China, huku Rais wa Taiwan akiapa kuwa katu haitokubali shinikizo la China.

Ubalozi wa China nchini Marekani haukutoa kauli yoyote maramoja. Marekani ilikatiza mahusiano na Taiwan baada ya aliyekuwa Rais wa Marekani Jimmy Carter kuitambua rasmi Beijing kuwa serikali pekee ya China mnamo mwaka wa 1978 na kuanzisha sera iliyojulikana kama "China Moja" mnamo mwaka wa 1979. Ubalozi wa Marekani ulifunga milango yake mjini Taipei mwaka wa 1979. China inakataa kuitambua Taiwan kama taifa huru na inapinga mahusiano yoyote yaliyo rasmi na taifa hilo

Ned Price, msemaji wa Baraza la Usalama wa Kitaifa katika Ikulu ya White House, amesema mazungumzo hayo hayatasababisha mabadiliko yoyote kwa sera ya muda mrefu ya Marekani kuhusu masuala ya China na Taiwan. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Taiwan Jumamosi ilisema kuwa Tsai alipokea simu na kiongozi wa Baraza la Usalama wa Kitaifa Joseph Wu na Waziri wa Mambo ya Kigeni David Lee. Simu hiyo iligusia mahusiano kati ya nchi hizo mbili na kuweka ushirikiano wa karibu. Tsai na Trump pia walijadili namna ya kukuza maendeleo ya kiuchumi ya ndani ya nchi na kuimarisha ulinzi wa kitaifa ili raia waweze kufurahia maisha bora na usalama.

Trump pia alifanya mazungumzo ya simu na Durtete
Trump pia alifanya mazungumzo ya simu na DurtetePicha: Reuters/R. Ranoco/W. Philpott

Wakati wa msimu wa uchaguzi, washauri wa Trump walitoa wito wa kuuziwa silaha Taiwan ili kukabiliana na nguvu za kijeshi za China zinazoendelea kukua, ijapokuwa anasema hajatunga sera halisi kuhusiana na Taiwan. Trump anatarajiwa kuchukua rasmi madaraka Januari. Tsai amekuwa rais wa Taiwan tangu Mei 20.

Trump pia alizungumza siku ya Ijumaa kwa njia ya simu na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte katika kile msaidizi mmoja wa Duterte alisema kuwa ni "mazungumzo mazuri sana”. Viongozi wote walialikana kuitembelea nchi ya kila mmoja wao mnamo mwaka wa 2017. Katika video iliyotolewa na msaidizi wa Duterte Bong Go, kiongozi huyo wa Ufilipino anaonekana akitabasamu wakati akizungumza na Trump. Timu ya mpito ya Trump haikutoa taarifa yoyote kuhusu mazungumzo hayo na haikubainika kama Trump alikubaliana na sera kali ya Duterte kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya watu waliotuhumiwa kuuza na kutumia dawa za kulevya.

Ufilipino ni mshirika muhimu wa Marekani katika Mashariki ya Asia, ijapokuwa mahusiano yamevurugika tangu Duterte alipochukua madaraka mwezi Juni. Duterte alimuita Rais wa sasa wa Marekani "mwana wa uasherati” na akamwambia "aende kuzimu” ikiwa ataitembelea Ufilipino. Aidha Duterte alitishia kuvunja mahusiano ya miongo mingi na Marekani na badala yake kufanya kazi na China.

Mwandishi: Bruce  Amani/kbd/gsw (AP, dpa, Reuters)
Mhariri: Yusra Buwayhid