1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atumia matusi kuhusu Haiti na nchi za Afrika

12 Januari 2018

Rais Trump ametumia neno la matusi dhidi ya Haiti na nchi za Afrika alipouliza swali la ni kwa nini Marekani iwapokee wahamiaji kutoka mataifa yaliyooza kama Haiti na ya Afrika

https://p.dw.com/p/2qjvT
USA - Präsident Trump PK
Picha: Getty Images/M. Wilson

MMT J2 12.01 Trump decries immigration from 'shithole countries' - MP3-Stereo

Rais wa Marekani Donald Trump ametumia neno chafu la matusi kuzungumzia juu ya Haiti na nchi za bara la Afrika. Katika mkutano wake na wabunge kuhusu mageuzi kuhusu suala la uhamiaji, Trump alitaka kujua ni kwa nini Marekani iwapokee wananchi kutoka katika mataifa yaliyooza.

Kwenye kikao na wabunge ikulu ya Marekani, Trump aliuliza swali kwa nini Marekani iwapokee wahamiaji kutoka katika mataifa yaliyooza kama Haiti na ya Afrika badala ya kuwapokea wahamiaji wanaotoka nchi kama Norway?

Maneno hayo yaliyoripotiwa kwanza na jarida la habari la Washington Post, yalizusha ghadhabu miongoni mwa Wademocrats na Warepublicans, na yamefufua maswali Kuhusu mazowea ya Rais Trump kutoa matamshi ya kibaguzi.

Umoja wa Afrika waishutumu kauli ya Trump

Baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika hawajayakosoa matamshi ya Trump
Baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika hawajayakosoa matamshi ya TrumpPicha: picture-alliance/dpa/K. Tlape

Kauli ya Trump ilikuja wakati wa kujadili mkataba uliopendekezwa wenye nia ya kuwazuia wahamiaji kupeleka familia zao nchini humo. Na pia ugeuze mpango wa Green card kutumika tu kuwapa kinga maelfu kwa maelfu ya wahamiaji vijana dhidi ya kurudishwa nyumbani kwao.

Umoja wa Afrika AU umesema umeshtushwa na kusikitishwa na matamshi ya matusi ya Trump. Msemaji wa Umoja huo Ebba Kalondo ameliambia shirika lahabari la Associated Press wanaamini kauli kama hizo zinahujumu maadili ya kimataifa, haki za binadamu na hali nzuri ya kuelewana.

Baadhi ya raia wa Haiti wanamtaka Trump kuomba radhi Afrika na Haiti

Maneno hayo pia yamekosolewa vikali na baadhi ya raia wa Haiti. Akiwemo mwanaharakati kwa jina Rene Civil ambaye amemtaja Trump kuwa sawa na saratani duniani kote na kwa nchi yake, na mtu anayesababisha mgawanyiko miongoni mwa watu.

"Tunamtaka Donald Trump kuomba radhi kwa bara zima la Afrika na kwa Haiti, nchi ambayo damu ya watu wake ilitumika kupitia mababu walioikomboa Marekani kutoka utumwani."

Wademocrats wamemkosoa Trump kuhusu matamshi yake ya matusi dhidi ya raia wa Haiti na Waafrika kwa kile walichosema kuwa yanaonesha anawapinga wahamiaji. Mbunge Luis Gutierrez wa Marekani amesema wanaweza kusema kuwa wanajua kwa asilimia 100 kuwa Rais Trump hawapendi watu kutoka baadhi ya nchi au watu wenye rangi fulani ya ngozi.

raia wa Haiti wameyakosoa matamshi ya Trump
raia wa Haiti wameyakosoa matamshi ya TrumpPicha: AP

Viongozi Afrika wakijuta njia panda

Serikali za nchi za Afrika zimejikuta njia panda kuhusiana na matamshi ya Trump. Kama wanaonufaika pakubwa kutokana na misaada ya Marekani baadhi zimeamua kunyamaza kimya kwani kumkosoa Trump kunaweza kuathiri misaada hasa ikizingatiwa utawala wa Trump umeamua kupunguza misaada.

Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini Ateny Wek Ateny ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa maadamu jina la Sudan Kusini halikutajwa, hawana la kusema.

Nchini Kenya, mwanaharakati wa kisiasa Boniface Mwangi amemsihi Trump atafautishe baina ya viongozi wachafu ambao Waafrika wenyewe huwachagua na bara linalopendeza la Afrika

Ikulu ya White House haikuyakana matamshi hayo ya matusi. Badala yake ilisema Trump ananuia kuifanya nchi kuwa imara kwa kuhakikisha kuna mfumo wa uhamiaji unaozingatia ufanisi.

Mwandishi: John Juma/AP/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu