Trump atoka hospitali, arejea Ikulu ya Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.10.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump atoka hospitali, arejea Ikulu ya Marekani

Rais wa Marekani, Donald Trump ameruhusiwa kutoka kwenye hospitali ya kijeshi ya Walter Reed alikokuwa amelazwa kwa siku tatu akitibiwa ugonjwa wa COVID-19.

Baada ya kuwasili kwenye Ikulu ya Marekani, White House, Trump alivua barakoa yake kwa ajili ya kupiga picha na aliendelea kutembea bila barakoa wakati wafanyakazi wa ikulu walipomkaribia kumsalimia. Mapema jana, rais huyo wa Marekani alitangaza kuwa ataondoka kwenye hospitali hiyo iliyoko Maryland, karibu na Washington D.C. Katika ukurasa wake wa Twitter, Trump aliweka ujumbe wa video akisema kwamba anajisikia vizuri sana.

''Nimeondoka kwenye hospitali ya Walter Reed, ni jambo la kipee sana. Nimejifunza mengi kuhusu virusi vya corona. Na jambo moja la uhakika, usiviache viyatawale maisha yako, usiviogope, utavishinda. Tuna vifaa bora kabisa vya matibabu. Na sasa najisikia vizuri. Asanteni sana,'' alisema Trump.

Tokeni nje

Trump amewataka Marekani watoke nje, lakini wahakikishe wanakuwa waangalifu, kwani ni lazima wavishinde virusi vya corona. Hata hivyo, madaktari wa Trump wamesema kiongozi huyo ataendelea na matibabu yake akiwa kwenye ikulu hiyo na kwamba bado anaweza kuwaambukiza watu wengine

Bado haijajulikana Trump ataendelea kukaa karantini kwa muda gani. Kabla ya kuondoka hospitali, Trump aliahidi kwamba atarejea kwenye kampeni hivi karibuni. Kulingana na Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa, watu wenye dalili ndogo na za wastani wanaweza kuambukiza kwa takriban siku 10, hivyo wanatakiwa kuendelea kujitenga.

Aidha, mgombea wa urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden amemtaka Trump kusikiliza na kuuzingatia ushauri wa madaktari. Biden ambaye Jumatatu aliendelea na kampeni, amesema atashiriki katika mdahalo wa pili wa urais na Trump uliopangwa kufanyika Oktoba 15, iwapo wataalamu wa afya watasema ni sawa kufanya hivyo. Biden alikutwa hana virusi vya corona baada ya kupimwa kwa mara ya pili siku ya Jumapili.

USA I Kayleigh McEnany I Coronavirus

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Kayleigh McEnany

Wakati huo huo, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Kayleigh McEnany naye ameambukizwa virusi vya corona na anajiweka katika karantini, lakini amesema ataendelea kufanya kazi kwa niaba ya watu wa Marekani.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang Schauble amesema wabunge watalazimika kuvaa barakoa wakiwa ndani ya maeneo ya bunge kuanzia siku ya Jumanne, kutokana na kuongezeka kwa visa vya virusi vya corona nchini humo. Schauble amesema barakoa zitavuliwa tu katika vyumba vya mikutano ikiwa agizo la kukaa umbali wa mita 1.5 litazingatiwa.

Takwimu za maambukizi zilizotolewa Jumanne na Taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukizwa ya Ujerumani, Robert Koch zinaonyesha kuwepo visa vipya 2,639 na vifo 12.

IMF yazisaidia nchi masikini

Nalo Shirika la Fedha Duniani, IMF limeidhinisha msaada mpya wa dharura kwa nchi 28 masikini duniani zikiwemo ili kuzisaidia kupunguza madeni yao na kukabiliana vizuri na athari za janga la virusi vya corona. Nchi zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Afghanistan, Tanzania, Ethiopia, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Djibouti, Benin, na Burkina Faso.

Nchi nyingine ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Comoro,  Gambia, Guinea, Guinea-Bissau, Haiti, Liberia, Madagascar, Malawi, Msumbiji, Nepal, Niger, Sao Tome na Principe, Sierra Leone, Visiwa vya Solomon, Tajikistan, Togo na Yemen.

Ama kwa upande mwingine, Kamishna wa Masuala ya Kiuchumi wa Umoja wa Ulaya, Paolo Gentiloni amesema sheria za umoja huo ambazo zinaweka mipaka kwa serikali kukopa, zitaendelea hadi mwaka 2021 kutokana na kuporomoka kwa uchumi kulikosababishwa na janga la virusi vya corona. Tangazo hilo limetolewa baada ya Gentiloni kukutana na mawaziri wa fedha wa nchi za ukanda unaotumia sarafu ya Euro mjini Brussels.

(AFP, DPA, AP, Reuters)