1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel

Isaac Gamba
7 Desemba 2017

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza rasmi kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel licha ya uamuzi huo kupingwa na viongozi kadhaa wa kidunia.

https://p.dw.com/p/2ouK1
Jerusalem Felsendom
Picha: DW/T. Krämer

 Kufuatia tangazo hilo la Trump ubalozi wa Marekani  sasa utahamishwa kutoka mjini Tel Aviv na kupelekwa Jerusalem.

Akizungumza hapo jana Jumatano katika ikulu ya Marekani White House Trump alisema  ni muda muafaka sasa kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuongeza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kutambua ukweli uliopo kuhusiana na suala hilo.

Licha ya kuonywa mara  kadhaa dhidi ya hatua hiyo na viongozi wa mataifa ya kiarabu  pamoja na viongozi wa ulaya ,  Trump amesema anaelekeza serikali yake kuanza matayarisho ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kuupeleka  Jerusalem. Amesema   anafanya hivyo kwa kuzingatia  sheria ya mwaka 1995 inayoelekeza Marekani kuhamishia ubalozi wake Jerusalem. 

Amesema wakati alipoingia madarakani  aliahidi kuangalia kwa makini changamoto zinazoikabili dunia na kuwa hauwezi kutafuta suluhisho la matatizo kwa kutumia njia zilezile zilizoshindwa wakati uliopita na kuongeza kuwa changamoto zozote zinahitaji  mtizamo mpya.

USA Trump erkennt Jerusalem als Hauptstadt Israels an
Rais wa Marekani Donald Trump na Makamu wake Mike PencePicha: Reuters/K. Lamarque

Aidha Trump ameongeza kuwa wakati marais waliopita walilifanya suala hilo  kama ahadi kubwa kwenye kampeni zao lakini walishindwa kutekeleza  ila kwa upande wake  sasa anatekeleza.

Akizungumzia uamuzi huo wa Trump Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema tangu siku ya kwanza kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akipinga   hatua zozote zinazoweza kuvuruga mchakato wa kuleta amani kati ya Israel na Palestina na kuwa  suala linalohusu Jerusalem  linapaswa kujadiliwa kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande zote mbili  za Israel na Palestina kwa kuzingatia maazimio ya  baraza  la usalama la Umoja wa Mataifa na hakuna mpango mbadala zaidi ya suluhisho la mataifa mawili.

USA UN-Vollversammlung in New York | Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Reuters/L. Jackson

Kwa upande wake rais wa Mamlaka ya ndani ya  Palestina  Mahmoud Abbas amesema kwa tangazo hilo la Trump  Marekani sasa inaonekana imejiondoa katika juhudi za kutafuta amani ya Israel na Palestina ambazo imekuwa ikizisimamia .  Katika hotuba yake alioitoa kwa njia ya Televisheni Abbas  amesema uamuzi huu wa Trump hautabadilisha ukweli kuhusu Jerusalem kwasababu ni mji wa wakristo na waislamu na mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina.  Aidha mapema hapo jana  Jumatano baadhi ya wapalestina waliandamana  ikiwa ni  pamoja na kuchoma moto bendera za Marekani na Israel kupinga  hatua ya Marekani kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Naye rais wa Ufaransa Emanuel Macron amesema  uamuzi wa Trump unakwenda kinyume na sheria ya kimataifa na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Macron amesema hadhi ya Jerusalem inapaswa kuamuliwa na waisrael na wapalestina katika mazungumzo yatakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu katika taarifa yake amesema  tangazo hilo la Trump ni hatua muhimu katika mchakato wa amani.

 Ama kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ameshutumu uamuzi huo wa rais Donald Trump na kusema ni uamuzi  ambao haukupaswa kutolewa.

Urusi mwanzoni mwa mwaka huu ilitangaza kuwa inalitambua eneo la magharibi mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na siyo eneo la mashariki ambalo linakaliwa na Israel.

Wakati huohuo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajia kukutana katika kikao cha dharula ikiwa ni baada ya Trump kutoa tangazo la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Mwandishi: Isaac Gamba/ dw/dpae/ape/rtre