1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asusia kikao, asema hatoshirikiana na Democrats

Lilian Mtono
23 Mei 2019

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kutoshirikiana na WaDemocrats, hadi watakapoachana na uchunguzi wa baada ya matokeo ya ripoti ya Robert Muller kuhusu mahusiano yake na Urusi katika uchaguzi wa 2016.

https://p.dw.com/p/3Ivxj
USA Washington Nancy Pelosi
Picha: picture-aliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Rais Donald Trump Ametangaza hatua hiyo baada ya kutoka ghafla kwenye kikao cha viongozi wa bunge jana Jumatano. 

Vita vya maneno vimezuka kati ya viongozi Rais Donald Trump na spika wa bunge Nancy Pelosi kuhusu kuimarishwa kwa uchunguzi wa bunge dhidi ya rais anayedaiwa kujihusisha na kuyakingia kifua baadhi ya madai, alisema "Ukweli uko wazi huyu rais anazuia upatikanaji wa haki na anajihusisha na kukingia kifua na hilo ni kosa la kutiliwa shaka na hata kuondolewa mamlakani."

Trump anayekaribia kuanza kampeni za kuomba kura katika uchaguzi wa mwaka 2020 ili kurejea kwa awamu ya pili amesema hatafanya kazi na Wademocrats, na hususan katika masuala yahusuyo miundombinu, ambayo ni miongoni mwa masuala machache ambayo baadhi wanaamini kwamba yanahitaji ushirikiano wa vyama vyote viwili, kutokana na kile anachodai ni madai ya uongo.

USA Donald Trump Rede an die Nation in Washington
Rais Donald Trump akipeana mkono na spika wa bunge, Nancy Pelosi alipohutubia kuhusu hali ya taifa mapema mwaka huu.Picha: Reuters/The New York Times/D. Mills

Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi ameita hatua hizo za Trump kuwa ni za kushangaza sana, na kusema amekuwa akimuombea Trump na taifa hilo. Kujibu hilo, Trump aliandika kwenye twitter akimshukuru Pelosi kwa sala zake lakini akisema asingeweza kuendelea katika mazingira hayo.

Mzozo huu unayaweka rehani masuala muhimu ya Trump kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

Alisema kwa waandishi wa habari "Nancy Pelosi, kabla tu ya mkutano wetu alisema kwamba wanaamini rais wa Marekani anajihusisha na kukingia kifua.. Sawa, lakini ni wazi... na nyinyi mtakubaliana nami kwamba mimi ndio rais muwazi zaidi, labda katika historia ya taifa hili."

Wakati mzozo huu ukionekana kuwa na faida ya muda mfupi kwake, huku matamshi yake yakiwafurahisha wafuasi wake, lakini unaiweka hatarini mikakati yake ya kibiashara, bajeti mpya na masuala mengine katika hatari wakati ambapo anatarajia kuanza kampeni ya kuomba ridhaa ya kurejea mamlakani, mwaka 2020.

Trump na Democrats ambao kwa pamoja wana udhibiti kwenye baraza la wawakilishi wako katika mvutano mkali kuhusu uwezo wa kimamlaka wa kumchunguza, huku rais Trump mwenyewe akizidi kusisitiza kwamba washauri wake hawatakiwi kuitikia miito ya wabunge kwa ajili ya kuchunguzwa.

Spika Pelosi amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna aliye juu ya sheria, ikiwa ni pamoja na rais wa Marekani. Siku ya Jumanne, kamati ya mahakama ya bunge ilitoa hati mbili za kuwaita na kuwahoji watumishi wa zamani wa ikulu ya White House, ikiwa ni pamoja na mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano, aliyekuwa karibu na Trump.