1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema yuko tayari kukutana na Iran

Bruce Amani
31 Julai 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kukutana na viongozi wa Iran bila masharti yoyote, kujadili namna ya kuimarisha mahusiano baada ya kuiondoa Marekani kutoka mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka wa 2015. 

https://p.dw.com/p/32MOp
Bildkombo - Trump und Rohani

Akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte aliyemtembelea katika Ikulu ya White House, Trump alisema kuwa yuko tayari kukutana na viongozi wa Iran kama nao watataka kukutana naye. "Ntakutana na yeyote. naamimi katika mikutano. kuzungumza na watu wengine, hasa wakati unazungumza kuhusu uwezekano wa kutokea vita na vifo na njaa na mambo mengine mengi. hakuna kitu kibaya katika kukutana".

Matamshi hayo yanajiri wakati Marekani ikijiandaa kwa kile inachokieleza kuwa ni vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran kufuatia uamuzi wa Trump wa mapema mwaka huu wa kuiondoa Marekani katika mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani.

Katika kujibu, Iran imesema njia pekee ya mazungumzo ni kwa Marekani kurejea katika muafaka huo wa nyuklia. Mshauri wa Rais wa Iran Hassan Rouhani, Hamid Aboutalebi ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa hatua zitakazowezesha kuanzishwa tena mazungumzo hayo magumu ni kuheshimu haki za taifa la Iran, kupunguza uhasama na kurejea katika mkataba wa nyuklia.

Ikulu ya Marekani imesema hata ingawa rais yuko tayari kwa mazungumzo, haina maana kuwa Marekani itaondoa vikwazo au kuanzisha tena mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani Mike Pompeo alifafanua kauli za Trump akitoa hatua tatu ambazo Iran lazima izizingatie kabla ya kufanyika mazungumzo. Alisema Wairan wanapaswa kuonyesha nia ya kuwa tayari kufanya mabadiliko muhimu ya namna wanavyowashughulikia watu wake, wapunguze tabia ya kuwachafulia watu jina na wakubali kuingia katika makubaliano ya nyuklia ambayo hakika yanazuia kuenea kwa silaha.

Mwaliko wa Trump unakuja baada ya onyo la kichochezi wiki iliyopita kutoka kwa Rais Rouhani, aliyesema kuwa Marekani haipaswi kuchezea mkia wa simba na akaonya kuwa mgogoro wowote na Iran utakuwa mama wa vita vyote.

Trump alijibu katika maandishi ya herufi kubwa kwenye Twitter akisema "usiwahi kuichezea tena Marekani au utapatwa na madhara ambayo ni wachache waliowahi kuyashuhudia katika historia yao."

Trump jana alimkaribisha katika Ikulu Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ambapo walielezea mshikimano wao kuhusu masuala ya uhamiaji. Kuhusu uhamiaji, Conte alisema

Viongozi hao walionyesha dalili za kuungana katika wakati ambapo Marekani imeharibu mahusiano yake na viongozi wa Ulaya. Trump alimpongeza Conte kwa kuchukua msimamo imara kwenye mipaka ya nchi akiongeza kuwa Marekani na Italia zitaanzisha ushirikiano mpya wa mazungumzo kuhusu masuala ya usalama, ugaidi na uhamiaji.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri:Josephat Charo