Trump asaini sheria kuwekea China vikwazo kuhusu Hong Kong | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump asaini sheria kuwekea China vikwazo kuhusu Hong Kong

Rais Trump amesaini sheria kuwawekea maafisa wa China vikwazo kuhusiana na matendo yao ya ukandamizaji dhidi ya Wahong Kong. Trump pia amesaini amri ya kumaliza uhusiano wa Marekani unaoipendelea Hong Kong.

Sheria aliyosaini Trump pamoja na amri ya rais, ni sehemu ya mashambulizi ya utawala wa Trump, dhidi ya China kuhusu kile anachosema ni matendo yasiyo sawa ya taifa hilo la Asia.

Shutuma hizo za karibu kila siku, za Trump dhidi ya China, zimejiri mnamo wakati Trump akijitetea dhidi ya ukosoaji kuhusu anavyolishughulikia janga la corona huku kukiwa na ongezeko la maambukizi mapya nchini mwake.

"Sheria hii inaupa utawala wangu zana mpya zenye nguvu kuwawajibisha watu na taasisi ambazo zimehusika kuipokonya Hong Kong uhuru wake. Sote tumeona kile kilichofanyika. Si hali nzuri. Uhuru wao umechukuliwa, haki zao zimechukuliwa, na kwa maoni yangu kutokana na hayo Hong Kong haipo kwa sababu, haitaweza tena kushindana na masoko huru.” Amesema Trump.

Sheria ya usalama wa China kwa Hong Kong yazusha wasiuwasi

China kulipiza kisasi!

Maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji Hong Kong Julai 1, 2020. Waandamanaji walipinga sheria mpya ya usalama wa taifa ya China kwa Hong Kong wanayosema itakandamiza uhuru wa kujieleza.

Maafisa wa polisi wakiwakamata waandamanaji Hong Kong Julai 1, 2020. Waandamanaji walipinga sheria mpya ya usalama wa taifa ya China kwa Hong Kong wanayosema itakandamiza uhuru wa kujieleza.

China tayari imesema italipiza kisasi dhidi ya hatua hiyo ya Trump, itakayoruhusu pia mabenki kuwekewa vikwazo kuhusiana na hatua yake dhidi ya Hong Kong.

Kwenye taarifa, wizara ya Mambo ya nchi za nje ya China imesema kipengee cha sheria ya Hong Kong kuhusu utawala wa ndani kinaikosea heshima sheria ya taifa kuhusu usalama, ambayo China iliuwekea mji huo  hivi karibuni.

Wizara hiyo imeongeza kwamba China itatoa majibu yanayostahiki ili kuyalinda masilahi ambayo ni halali, na pia itaweka vikwazo kwa maafisa wa Marekani na kampuni zake.

Muswada ambao Rais Trump amesaini kuwa sheria unavilenga vikosi vya polisi ambavyo vimewakandamiza waandamanaji wa Hong Kong, pamoja na maafisa wa Chama cha Kikomunisti kinachotawala China wanaohusishwa na sheria ya taifa ya usalama wa China kwa Hong Kong, inayotizamwa kupunguza nguvu ya utawala wa ndani wa Hong Kong.

Mabenki pia kulengwa kwenye vikwazo vya Marekani

Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya China yasema, Beijing italipiza kisasi dhidi ya hatua za Trump.

Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya China yasema, Beijing italipiza kisasi dhidi ya hatua za Trump.

Hong Kong chini ya kiwingu cha sheria mpya ya usalama

Sheria hiyo inataka vikwazo vya lazima kuwekewa pia mabenki ambayo yanafanya biashara na maafisa watakaowekewa vikwazo.

Uhusiano kati ya Marekani na China umekuwa mbaya zaidi, tangu mataifa hayo mawili yaliposaini awamu ya kwanza ya makubaliano ya biashara lakini hadi sasa mazungumzo hayo yamekwama.

Wabunge wa pande kuu mbili za kisiasa nchini Marekani, wamemhimiza Rais Trump kuchukua hatua kali dhidi ya China kuhusiana na sheria hiyo ya usalama wa taifa iliyoiwekea Hong Kong, ambayo inapunguza nguvu ya makubaliano ya kuwepo "nchi moja lakini mifumo miwili" wakati Uingereza ilipoikabidhi Hong Kong kwa China mwaka 1997.

Vyanzo: APE/AFPE