Trump apiga marufuku wasafiri kutoka Brazil | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Marekani yapiga marufuku wasafiri kutoka Brazil

Trump apiga marufuku wasafiri kutoka Brazil

Katika juhudi za kupamba na mripuko wa virusi vya corona rais wa Marekani Donald Trump amepiga marufuku wasafiri kutoka Brazil. Wakati huo huo rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameshusha kiwango cha kitisho.

Afisa habari wa Ikulu ya White House mjini Washington Kayleigh McEnany amesema kuanzia Alhamis wiki hii, watu wote wasio raia wa Marekani ambao wamekuwa nchini Brazil katika muda wa majuma mawili yaliyopita, hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni juhudi ya kuepusha maambukizi mapya kutoka nje ya nchi.

Marufuku hiyo haitawahusu raia wa Marekani wanaorejea nyumbani, na pia wale wenye vibali vya kudumu vya kuishi nchini humo.

Bolsonaro aendelea kutojali

Brazil ambayo hivi sasa inavyo visa vipatavyo 367,000 vya corona na imerikodi vifo zaidi ya 22,000 kutokana na virusi hivyo, ipo katika nafasi ya pili kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya COVID-19, ikitanguliwa tu na Marekani.

Brasilien | Coronavirus

Brazil hivi sasa ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na maambukizi mengi ya virusi vya corona baada ya Marekani

Licha ya hali hiyo, Rais wa Brazil Jair Bolsonaro anaendelea kuubeza mripuko wa janga hilo la corona, akishikilia kuwa ni mafua ya kawaida. Wizara ya mambo ya nje ya Brazil imesema haikuipa umuhimu mkubwa marufuku hiyo ya safari ya Marekani, ikiitaja kuwa ni mchakato wa kawaida wa tahadhari.

Afrika Kusini yashusha kiwango cha kitisho cha corona

Huko Afrika Kusini, rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa ameshusha kipimo cha kitisho kitokanacho na janga la corona kutoka ngazi ya tatu hadi ya tatu, na kusema marufuku dhidi ya mauzo ya pombe yatalegezwa, na kuruhusu mauzo ya bidhaa hiyo kwa wale wanaotaka kunywa wakiwa nyumbani. Ramaphosa amesema kushusha kiwango cha kitisho cha corona ni hatua muhimu.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

''Kuingia katika ngazi ya tatu ya kitisho ni mabadiliko makubwa katika mkakati wa kupambana na janga hili. Kutaruhusu kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya sekta mbali mbali za uchumi na safari za watu, huku tukiimarisha shughuli za kulinda afya ya umma.'' Amesema Rais Ramaphosa.

Hata hivyo Rais Ramaphosa amesema marufuku dhidi ya mauzo ya sigara na tumbaku itabakia pale pale.

Akufaaye kwa dhiki...

Kwingineko, meya wa jiji la Berlin hapa Ujerumani Michael Mueller amesema hospital za mji huo ziko tayari kujitolea kuwapokea wagonjwa wa corona kutoka mjini mkuu wa Urusi, Moscow ambao mfumo wake wa afya umelemewa.

Mueller ameliambia gazeti la Die Tagesspiegel Jumapili, kwamba tayari hospitali za Berlin zimewasaidia wagonjwa kutoka Ufaransa, na zilikuwa tayari kuisaidia Italia iwapo ingekuwa na mahitaji hayo. Urusi ni nambari tatu duniani kwa maambukizi ya COVID-19, ikiwa na visa 344,000 na vifo zaidi ya 3,500.

 

dpae, afpe