Trump aondoka kwa hasira mazungumzo kuhusu ukuta | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump aondoka kwa hasira mazungumzo kuhusu ukuta

Mvutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa chama cha Democratic kuhusu ujenzi wa ukuta wa mpakani unaotakiwa na rais huyo, umeingia sura mpya baada ya Trump kuondoka kwa hasira kwenye mazungumzo.

Tofauti kuhusu ukuta huo kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico, ambao umekataliwa katakata na wademocrats, umesababisha kufungwa kwa wizara na idara kadhaa za serikali kwa muda wa siku kumi na tisa sasa. 

Mkutano baina ya Rais Trump na viongozi wa chama cha Democratic bungeni, Nancy Pelosi ambaye ni spika wa baraza la wawakilishi na Chuck Schumer, kiongozi wa wademocrats katika baraza la seneti, haukudumu kwa muda mrefu.

Mazungumzo baina yao yalikuwa yakijaribu kwa mara nyingine kutafuta muafaka wa kumaliza mkwamo wa shughuli za serikali, ulioanza siku 19 zilizopita baada ya Trump kukataa kusaini mpango wa bajeti ambao haujumuishi dola bilioni 5.7 anazozitaka kwa ajili ya ujenzi wa ukuta katika mpaka baina ya Marekani na Mexico, ambao ni ahadi yake kuu ya kampeni yake ya urais.

Trump aliarifu kilichojiri katika mazungumzo hayo mafupi, kupitia ukurasa wake wa twitter. Amesema na hapa nanukuu, ''nimeondoka sasa hivi katika mkutano na Chuck na Nancy, ambao ulikuwa ni kupoteza muda kabisa. Nimewauliza ikiwa nitazifungua haraka shughuli za serikali, kipi kitafanyika katika siku 30 zitakazofuata, mtaridhia fedha za kujenga ukuta mpakani, Nancy akajibu 'hapana', nikawaambia, 'kwa heri, hakuna kitakachofanyika hapa'.

Wademocrats wapigwa butwaa

Wademocrats waliopigwa na butwaa wamesema tabia ya Rais Donald Trump ni mhemuko wa ghadhabu. Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi amesema rais wa Marekani ameonyesha tabia ya kitoto. ''Mtu ambaye anasema, nitazifunga shughuli za serikali kwa wiki, miezi hata miaka ikiwa matakwa yangu hayataridhiwa, huo sio utendaji kazi wa kidemokrasia, ni hali ya kusikitisha.'' amesema Pelosi baada ya mazungumzo hayo yaliyovunjika.

Chuck Schumer amewaambia waandishi wa habari kwamba wao kama wademocrat wana imani katika ulinzi imara wa mpaka, na wanataka kupata makubaliano, ingawa wana mtazamo tofauti na rais Trump kuhusu namna ya kulishughulikia suala hilo.

Kushindwa kwa mazungumzo kati ya pande hizo, kunasogeza karibu uwezekano wa Trump kutangaza hali ya dharura kitaifa, ambayo ataitumia kupata fedha za ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Kusini wa nchi, ikiwa bunge halitaruhusu bajeti anayoitaka.

Jana, Trump alisema anayo mamlaka ya kutangaza hali hiyo ya dharura na kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya wizara ya ulinzi kujengea ukuta wake wa mpakani. Makamu wake, Mike Pence, amewaambia waandishi wa habari kwamba rais huyo bado anatafakari hatua hiyo.

Pence alipoulizwa faida aliyoipata Trump kwa kujiondoa mkutanoni akiwaacha wenzake, amejibu kwamba Trump amekwisha eleza bayana msimamo wake, kwamba hakutakuwa na muafaka usiohusisha ujenzi wa ukuta.

Nani atalegeza kamba?

Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo baraza la wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Democratic lilipitisha mpango wa kuzifungua baadhi ya wizara ambazo hazifanyi kazi tangu Desemba 22, bila kutilia maanani ujenzi wa ukuta. Hata hivyo hakuna dalili kwamba mpango huo utapita katika baraza la seneti ambako warepublican wanayo kauli ya mwisho.

Wademocrat wanajaribu kuwasukumiza warepublican katika hali ya kuchagua kati ya kuridhia kufunguliwa kwa idara muhimu, ikiwemo ile inayohusika na kuwapa mamilioni ya walipa kodi marejesho yao wakati ukiwadia, au kushikamana na rais Trump katika kuendelea kuzifunga idara hizo.

Hapo jana Rais Trump alishiriki chakula cha mchana na wajumbe wa chama chake cha Republican katika baraza la seneti, na baadaye alisema maseneta hao wanaunga mkono kikamilifu msimamo wake mkali kuhusu ujenzi wa ukuta mpakani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, ape

Mhariri: Rashid Chilumba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com