Trump anatarajia vikosi vya Iraq vitaulinda ubalozi wake mjini Baghdad | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.12.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump anatarajia vikosi vya Iraq vitaulinda ubalozi wake mjini Baghdad

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema anatarajia Iraq itatumia vikosi vyake vya usalama kuulinda ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Kauli hiyo ameitoa wakati ambapo anailaumu Iran kwa kuchochea vurugu hizo dhidi ya eneo lake. Wananchi wa Iraq ambao ni wafuasi wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran waliandamana kwenye ubalozi wa Marekani siku ya Jumanne huku wakiimba nyimbo zinazosema ''Kifo cha Marekani,'' wakirusha mawe, wakivunja kamera za usalama pamoja na kulichoma moto eneo la mapokezi, wakilaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani.

Wapiganaji 25 waliuawa

Mashambulizi hayo yaliyofanyika Jumapili iliyopita yaliwaua wapiganaji wapatao 25 wa kundi la wanamgambo wa Kataeb Hezbollah. ''Tunatarajia Iraq itavitumia vikosi vyake kuulinda ubalozi na tumearifiwa hivyo,'' ameandika Trump katika ukurasa wake wa Twitter. Trump amesema Iran itawajibika kikamilifu kwa machafuko hayo.

Mashambulizi ya Marekani yalikuwa ni kujibu shambulizi la roketi lililofanywa wiki iliyopita na kumuua mkandarasi mmoja wa Kimarekani katika kituo cha jeshi la Iraq, ambalo ni la karibuni kufnayika lililenga maslahi ya Marekani nchini Iraq. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulizi hilo, lakini vikosi vya usalama vya Marekani vimelishutumu kundi la Kataeb Hezbollah.

Proteste bei der US-Botschaft in Baghdad

Wapiganaji wa kundi la Hashd al-Shaabi wakiwasha moto kwenye ukuta wa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad

Trump amesema Marekani imejibu vikali shambulizi ambalo limemuua mkandarasi huyo na skwamba siku zote itafanya hivyo. Uhusiano kati ya Marekani na Iran umekuwa ukizorota tangu Marekani ilivyojiondoa kwenye mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa Iran mwaka 2018 na kuweka vikwazo vipya.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kadhaa kwa waandamanaji kufanikiwa kuufikia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, uliopo kwenye eneo lenye ulinzi mkali maarufu kama Green Zone. Vikosi vya usalama ndani ya ubalozi huo walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji nje ya ubalozi huo. Imeripotiwa kuwa zaidi ya watu 20,000 walikusanyika nje ya ubalozi huo.

Hofu ya Iraq

Kwa muda mrefu Iraq imekuwa na hofu ya kuwa katikati ya mzozo wa Marekani na Iran ambao unaongezeka, ambazo zote mbili ni mshirika wake mkuu. Siku ya Jumatatu serikali ya Iraq ililaani vikali mashambulizi hayo ya mwishoni mwa wiki na kuonya kuwa huenda ukaathiri uhusiano wake na Marekani. Baadae Marekani iliishutumu Iraq kwa kushindwa kuyalinda maslahi ya nchi hiyo.

USA Washington | Außenminister Mike Pompeo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo

Hata hivyo, siku ya Jumanne viongozi wa Iraq walihakikisha kuhusu usalama wa maafisa wa Kimarekani pamoja na mali zao. Ahadi hiyo wameitoa walipozungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kwa njia ya simu, baada ya waandamanaji kuuvamia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Morgan Ortagus amesema Pompeo amezungumza kwa nyakati tofauti na Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul-Mahdi pamoja na rais wa nchi hiyo, Barham Salih. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pompeo ameweka wazi kwamba Marekani itawalinda na kuwatetea watu wake ambao wako Iraq kuunga mkono uhuru wa Iraq.

Ortagus amefafanua kuwa Abdul-Mahdi na Salih wamemuahidi Pompeo kwamba wanalichukua jukumu lao kwa umakini mkubwa na watahakikisha usalama wa watu wa Marekani pamoja na mali zao.

(AFP, DPA, AP, Reuters)