1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amshambulia Bannon

Iddi Ssessanga
4 Januari 2018

Ikulu ya Marekani imejibu kwa ukali matamshi yaliyotolewa na Steve Bannon, ikisema afisa huyo mtendaji wa zamani wa kampeni na mpanga mikakati mkuu wa Rais Donald Trump amepungukiwa na akili.

https://p.dw.com/p/2qJVH
Washington Präsident Trump Flynn und Bannon Oval Office at the White House
Trup akiwa na waliokuwa washauri wake waandamizi ofisini kwake - Michael Fylnn na Steve Bannon, Januari 28,2017.Picha: Reuters/J. Ernst

Vita hivyo vya maneno kati ya Rais Trump na msaidizi wake wa zamani vimesababishwa na dondoo kutoka kwenye kitabu kipya kilichopewa kichwa cha "Moto na Ghadhabu: Ndani ya Ikulu ya Trump" ambamo Bannon anautaja mkutano kati ya mtoto wa rais, Donald Trump Junior, mwenyekiti wa zamani wa kampeni Paul Manafort na mkwe wa Trump Jared Kushner na mwanasheria wa Urusi, kuwa wa kihaini na uliokosa uzalendo.

Matamshi hayo, yaliyomo kwenye kitabu kinachotarajiwa kutolewa hivi karibuni na kinachoelezea juu ya nyakati za mwanzo za urais wa Trump, pia kinamuhusisha Bannon akisema kwamba uchunguzi juu ya Urusi,  "unahusu utakatishaji fedha" na kwamba Mchunguzi Maalumu Mueller "atampasua Donald Junior kama yai."

Matamshi hayo yanawakilisha tukio la kwanza ambapo Trump anahusishwa moja kwa moja na mkutano na mwanasheria wa Urusi Natalia Veselnitskaya, aliekuwa ameahidi nyaraka ambazo zingemponza Hillary Clinton, wakati Bannon anapotaja kuwa "hakuna uwezekano wowote kwamba Rais hakufahamishwa juu ya jambo hilo.

USA | Steve Bannon
Rais Trump akifuatwa kwa nyuma na Steve Bannon alipokuwa mshauri wake wa juu, kabla ya Bannon kuondoka ikulu Agosti 2017.Picha: REUTERS/J. Ernst

Matamshi hayo mazito yamekuja wakati ambapo Paul Manafort amefungua kesi dhidi ya mchunguzi maalumu Robert Mueller siku ya Jumatano, akiiomba mahakama kupunguza uchuguzi wa Urusi. Trump amemshabulia Bannon na kusema kuwa hakupoteza tu kazi yake alipoondoka ikulu ya White House mwezi Agosti, lakini pia alipoteza na akili yake.

"Nadhani ghadhabu na kuchukizwa, ndiyo maneno yanayofaa kutumiwa pale mtu anapotoa madai ya kufedhehesha na tuhuma za uongo dhidi ya rais, utawala wake na familia yake," alisema msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sander katika mkutano na waandishi wa habari mjini Washington.

Maudhui ya kitabu

Kitabu cha "Fire and Fury: Inside the Trump White House", au "Moto na Ghadhabu: Ndani ya Ikulu ya Trump", kilichoandikwa na mwandishi habari Michael Wolf, kinahusisha mahojiano marefu na Bannon, ambaye sasa amerejea kuongoza tovuti ya habari inayoelemea siasa kali za mrengo wa kulia ya Breibart News.

Gazeti la Uingereza la The Guardian lilichapisha baadhi ya dondoo kutoka kwenye kitabu hicho ambamo Bannon aliuelezea mkutano uliofanyika katika jengo la Trump Tower kati ya maafisa wa kampeni ya Trump, akiwemo mwanae wa kiume Donald Trump Junior, na maafisa wanaohusishwa na ikulu ya Kremlin kama wa kihaini.

Wolfs anasema alimhoji Trump na duru nyingine zilizo karibu na rais huyo mwenye msimamo mkali wa kulia. Katika taarifa yake, Trump alisema alikuwa akikutana kwa nadra peke yake na Bannon, na amemlaumu kwa kushindwa kwa Mrepublican katika uchaguzi wa kiti cha Seneti katika jimbo la Alabama mwezi uliopita, na kukanusha pia kuwa alichagia chochote katika ushindi wake wa kihistoria, ambao anasema uliletwa na wanaume na wanawake wa nchi hiyo waliosahaulika.

Donald Trump Jr.
Mtoto wa Rais Trump, Donald Trump Junior.Picha: picture-alliance/AP/C. Kaster

Akana mchango wa Bannon katika mafanikio yake

Trump amemshutumu Bannon kwa kuvujisha "taarifa za uongo" kutoka Ikulu na kuwasaidia wanahabari kuandika kile alichokiita vitabu bandia, wakati alipokuwa ikulu alikuwa akionyesha kuvipiga vita vyombo vya habari na kuviita chama cha upinzani.

Wakati wa kampeni zake, mwanae Trump Jr. mkwe wake Jared Kushner na meneja wa zamani wa kampeni Paul Manafort, walifanya mkutano katika jengo la mgombea huyo lililoko Manhattan, pamoja na kundi la watu wenye uhusiano na serikali ya Urusi, ambao walidai kuwa na taarifa za kumharibia mpinzani wa Trump Hillary Clinton.

Makala tofauti iliyoandikwa na Wolf katika jarida la New York inasema Trump na washirika wake hawakutarajia kabisa kushinda uchaguzi wa 2016, na walipokea ushindi huo kwa mshtuko. Wolf amesema alifanya mahojiano zaidi ya 200 na wengi wa maafisa wa juu wa Trump na pia wa ndani wao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, afpe

Mhariri:Grace Kabogo