Trump amfuta kazi Mwanasheria Mkuu Sessions | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump amfuta kazi Mwanasheria Mkuu Sessions

Mwanasheria mkuu wa Marekani Jeff Sessions amejiuzulu baada ya kuombwa kufanya hivyo na rais Donald Trump, hatua inayoibua maswali juu ya hatma ya uchunguzi wa madai ya Urusi kuingilia katika uchaguzi wa 2016.

Kwenye barua aliyomwandikia rais Trump isiyo na tarehe, Sessions amesema kwamba, "nimepata heshima ya kufanya kazi kama mwanasheria mkuu na nimefanya kazi ya kutekeleza ajenda kulingana na misingi ya utawala wa sheria". Trump amemshukuru Sessions na kusema nafasi yake itashikiliwa kwa muda na Mathew Whitaker, aliyekuwa msaidizi wa Sessions. "Tunamshukuru mwanasheria mkuu Jeff Sessions kwa utumishi wake na kumtakia kila lenye kheri", Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.

Sessions mwenye miaka 71, seneta wa zamani wa jimbo la Alabama, alikuwa mfuasi wa kwanza kumuunga mkono Trump, lakini alichochea ghadhabu baada ya kujiondoa mwenyewe katika uchunguzi juu ya uingiliaji wa Urusi katika kampeni za urais.

Uamuzi huo ulimkasirisha Trump kwasababu asingekwepa uchunguzi wa shirikisho, unaotizama ka ukaribu ikiwa wasaidizi wa Trump, walikula njama na Urusi wakati wa kampeni zake. Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kutolewa miezi ya baadae. 

Trump ameapa kupambana na Wademocrat kama watatumia udhibiti wao kwenye baraza la wawakilishi kuanzisha uchunguzi katika utawala wake na fedha. Uamuzi wake wa kumfuta kazi Sessions umeibua ukosoaji kutoka kwa Wademocrat, wanaosema anatafuta kuudhofisha uchunguzi wa Urusi.

 USA: Jeff Sessions wurde entlassen (Reuters/J. Ernst)

Trump na Jeff Sessions wakiimba wimbo wa taifa

Kiongozi anayetazamiwa kuliongoza baraza la wawakilishi Nancy Pelosi, aliandika kwenye twitter kwamba kuondolewa kwa mwanasheria huyo ni hatua ya wazi ya kudhoofisha uchunguzi wa Urusi. Amemtaka Whitaker kujiweka kando na uchunguzi unaosimamiwa na mchunguzi maalum Robert Mueller. Seneta Chuck Schumer wa Democratic anasema uchunguzi huo unapaswa kulindwa na mabunge yote.

"Kwanza ninapata mashaka na muda wa tukio, Pili, mtazamo wetu ni kwamba mwanasheria yeyote, iwe huyu au mwingine asiingilie uchunguzi wa Mueller kwa namna yoyote. Wasijaribu kukomesha uchunguzi wala kuubinya. Wasijaribu kumwingilia Mueller ashindwe kusonga mbele na kufanya kile anachofikiria ni jambo sahihi".

Urusi wakati wote imekana kuingilia  uchaguzi wa Marekani, na Trump anadai uchunguzi wa Mueller ni kumsaka mchawi na amerejelea kusema hapakuwa na njama za aina yoyote.

Rais Trump anadai kwamba anao uwezo wa kumfukuza kazi Mueller kama angetaka lakini anasita kuchukua hatua kama hiyo, "ninaweza kumfuta kazi yeyote sasa lakini sitaki kusimamisha kwasababu kisiasa sitaki kusimamisha uchunguzi".

Rais Trump amesema yuko tayari kufanya kazi na Wademokcat katika vipaumbele muhimu lakini anahisi uchunguzi wowote kwenye utawala wake utaathiri matarajio ya ushirikiano wa vyama hivyo vya siasa.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com